Fikiri Elias aanza kwa kismati Coastal Union

KOCHA mpya wa Coastal Union, Fikiri Elias, ameanza vyema maisha yake ndani ya kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’, baada ya kushinda mechi mbili mfululizo za mashindano, tangu alipoteuliwa kuiongoza timu hiyo, Aprili 10, 2026.

Fikiri alifikia makubaliano ya kujiunga na kikosi hicho akichukua nafasi ya Mohamed Muya, aliyeondoka Aprili 8, 2026, kutokana na mwenendo mbaya, ambapo kocha huyo wa zamani wa KenGold FC ya jijini Mbeya, ameanza vyema maisha yake mapya.

Aprili 11, 2026, kocha huyo aliifunga Pamba Jiji mabao 2-0 katika raundi ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB na kufuzu robo fainali, kisha kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu akaichapa pia Dodoma Jiji mabao 3-1, Aprili 15, 2026. Ushindi wa mechi hizo mbili mfululizo, ni mara ya kwanza Coastal Union inafanya hivyo msimu huu kitendo ambacho Fikiri amekifanikisha akiwazidi watangulizi wake, Ali Mohamed Ameir na Mohamed Muya.

Akizungumzia mwenendo wa timu hiyo tangu amekabidhiwa, Fikiri amesema hakuna mabadiliko makubwa ya kiuchezaji aliyofanya hadi sasa, isipokuwa alichofanya ni kukaa na wachezaji na kuwajenga kiakili, kwa sababu nafasi ya kufanya vizuri wanayo. “Huwezi kubadilisha kila kitu kwa wiki moja, mechi mbili zimetuongezea morali kwa sababu unaposhinda hali ya kujiamini kwa wachezaji inarejea, jambo muhimu ni kuona tunazidi kuendeleza kiwango hiki bora tulichonacho sasa,” amesema Fikiri.

Kocha huyo alikuwa hana timu ya kuifundisha tangu alipoachana na KenGold FC, Septemba 17, 2024, kwa makubaliano ya pande mbili, baada ya mwenendo mbaya katika Ligi Kuu, jambo lililosababisha kushuka daraja na kucheza Ligi ya Championship msimu huu.

Msimu wa 2024-2025, Fikiri aliiongoza KenGold katika mechi tatu za Ligi na kupoteza zote, akichapwa mabao 3-1 dhidi ya Singida Black Stars (Agosti 18, 2024), kisha 2-1 dhidi ya Fountain Gate (Septemba 11, 2024) na kichapo cha bao 1-0 mbele ya KMC (Septemba 16, 2024).

Fikiri anakuwa ni kocha wa tatu msimu huu kuifundisha Coastal Union, baada ya awali kikosi hicho kuanza na Ali Mohammed Ameir, aliyeondoka Oktoba 1, 2025, kisha kuteuliwa Muya, Oktoba 6, 2025, naye aliondoka Aprili 8, 2026.