Siku 560 za Waziri Junior Dodoma Jiji

MSHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji, Waziri Junior, amehitimisha ukame wa siku 560 ambazo ni sawa na mwaka mmoja, miezi sita na siku 13, za kufunga bao la Ligi Kuu Bara, tangu mara ya mwisho kwa nyota huyo alipofunga Oktoba 2, 2024.

Nyota huyo amehitimisha ukame huo baada ya kuifungia Dodoma Jiji bao moja wakati kikosi hicho kilipochapwa mabao 3-1 dhidi ya Coastal Union, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Aprili 15, 2026 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Katika mechi hiyo, mabao ya Coastal Union yalifungwa na Greyson Gwalala dakika ya 14, Maabad Maulid (dk 32) na Jofrey Manyasi (dk 90+3), huku Waziri Junior akifunga bao pekee kwa Dodoma Jiji dakika ya 90+1.

Bao hilo dhidi ya Coastal Union, limemfanya nyota huyo kuhitimisha ukame wa siku hizo 560, ambapo kabla ya hapo mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni ushindi wa Dodoma Jiji wa mabao 2-0 dhidi ya TRA United zamani Tabora United, Oktoba 2, 2024.

Nyota huyo alirejea Dodoma Jiji Agosti 15, 2025, baada ya kuondoka Februari 7, 2025 kwenda kujiunga na Al-Minaa ya Ligi Kuu ya Iraq kwa mkopo wa miezi sita, ingawa ameanza kukitumikia kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari mwaka huu.

Sababu ya nyota huyo kuanza kukitumikia kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2026, ni baada ya Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kuchelewa kutoka, wakati akiichezea Al-Minaa, hivyo kukaa nje kwa miezi minne.

Msimu wa 2024-2025, haukuwa mzuri zaidi kwa nyota huyo kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, ingawa msimu bora kwake ni wa 2023-2024 alipokuwa KMC ambapo alishika nafasi ya tatu ya wafungaji bora, baada ya kufunga mabao 12.

Katika msimu huo, Waziri alizidiwa na kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mabao 19 na kinara Stephane Aziz KI, aliyekuwa Yanga kwa wakati huo aliyefunga 21, ingawa kwa sasa anacheza Al-Ittihad SC ya Libya.

Baada ya kuichezea Al-Minaa, mshambuliaji huyo ameandika rekodi pia akiwa ni Mtanzania wa pili kucheza soka la kulipwa Ligi Kuu ya Iraq, ambapo wa kwanza ni aliyekuwa nyota wa zamani wa Yanga, Saimon Msuva ambaye anaichezea Al-Talaba SC.