VURUGU kubwa zilizotokea katika dakika za nyongeza kwenye mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la FA Unguja kati ya Muembe Makumbi na JKU, zimefanya mchezo huo kuvunjika, huku waamuzi wakitolewa uwanjani kwa ulinzi mkali.
Mechi hiyo iliyochezwa Aprili 15, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, ilizuka vurugu kubwa baada ya wachezaji wa Muembe Makumbi kumvamia mwamuzi msaidizi, Abdallah Kombo aliyenyanyua kibendera kuashiria bao lililofungwa na mchezaji wa timu hiyo kwamba aliotea.
Tukio hilo lilitokea katika dakika sita za nyongeza baada ya kufika 90, huku JKU ikiwa mbele kwa mabao 2-1.
Mwanaspoti lililokuwepo uwanjani hapo, lilishuhudia tukio hilo ambapo wachezaji wa Muembe Makumbi waliona wamedhulumiwa bao lao la kusawazisha, ndipo wakamvamia mwamuzi kudai haki yao hali iliyofanya pia mashabiki na baadhi ya viongozi wa timu hiyo kuingia uwanjani kabla ya waliokuwa wakilinda usalama kuwaokoa waamuzi.
Matukio ya aina hiyo sio mara moja kutokea katika mechi za mashindano mbalimbali zinazochezwa uwanjani hapo huku Muembe Makumbi ikitajwa kuwa miongoni mwa timu zenye mashabiki wenye vurugu.
Novemba 14, 2025, Muembe Makumbi ilipocheza mechi ya Ligi Kuu Zanzibar dhidi ya KVZ, mashabiki wa timu hiyo walifanya vurugu jambo ambalo lilisababisha kuvunjika kwa mchezo kabla ya wakati.
Kutokana na vurugu hizo, timu hiyo ilitozwa faini ya Sh5 milioni na kulipa gharama zote za uharibifu wa miundombinu ya uwanja baada ya kukamilika kwa tathmini.
Adhabu hizo zilitolewa na Bodi ya Ligi Zanzibar chini ya sura ya 20 ya kanuni ya mashindano ya 2025-2026.
