Sh430 milioni zilivyosaidia elimu Bugurula

Geita. Zaidi ya wanafunzi 470 wa Shule ya Msingi Bugurula wilayani Geita Mkoa wa Geita waliokuwa wakilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita nane kila siku kwenda na kurudi shule, wameondokana na adha hiyo baada ya Serikali kutoa zaidi ya Sh330 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya.

Fedha hizo zilitolewa na Serikali mwaka 2025 na hivyo kusaidia ujenzi wa shule hiyo mpya ya Kigoma iliyojengwa katika Kijiji cha Bugurula na hivyo kufanya kijiji hicho kuwa na shule mbili za msingi, hali ambayo imesaidia pia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Bugurula.

Taarifa hiyo imetolewa kijijini hapo leo Alhamisi Aprili 16, 2026 na Katibu wa Shina la CCM namba 12 katika Kata ya Bugurula, Saidi Issa kwa Katibu wa Uenezi,Itikadi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi aliyepo mkoani Geita kwa ziara ya kichama.

Issa amesema kutolewa kwa fedha hizo kulifaniukisha ujenzi wa madarasa tisa katika shule hiyo, ambayo tayari imeanza kutoa huduma mwaka huu baada ya ujenzi huo kukamilika.

“Hii imetusaidia sana kwani watoto wetu walikuwa wanatembea umbali mrefu kuja shule mama, lakini pia kulikuwa na msongamano sana kwenye hii shule yetu,” amesema

Ameongeza kuwa Serikali pia imetoa zaidi ya Sh100 milioni kwa ajili ya ukarabati wa shule ya Msingi Bugurula kutokana na uchakavu wa miundombinu yake wa muda mrefu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bugurula, Peter Mihayo amesema kabla ya ujenzi wa shule mpya shule yake ilikuwa ikikabiliwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani.

Katibu Uenezi, itikadi na Mafunzo wa CCM,  Kenani Kihongosi akizungumza katika Shina namba 12 katika Kata ya Bugurula wilayani Geita Mkoa wa Geita.

“Shule ilikuwa na wanafunzi zaidi ya 2,300 hali iliyokuwa ikisababisha watloto zaidi ya 100 kukaa kwenye darasa moja lakini baada ya wanafunzi wengine kuhamasishwa kwenye shule mpya na shule yetu pia kufanyiwa ukarabati, hivi sasa hatuna msongamano na mazingira ya shule yamekuwa bora zaidi,” amesema.

Akizungumza katika mkutano huo wa shina, Kihongosi amesema ajenda kuu ya CCM ni kupeleka maendeleo kwa wananchi huku akiwataka wananchi kujiandaa kupokea miradi mingi ya maendeleo kwa masilahi ya wananchi wote.

Amewataka Watanzania wote kuendelea kulinda amani na utulivu nchini, ili Serikali ya CCM iweze kutekeleza mipango yake ya maendeleo kama ambavyo imepangwa.

“Serikali ya CCM hivi sasa inaendelea kupika mambo mazuri kwa ajili ya Watanzania wote, leo tunazungumzia elimu lakini jiandaeni kupata miradi mingi katika sekta zote kwaajili ya maendeleo ya wananchi,” amesema

Amesema mipango hiyo ya maendeleo itatakelezwa endapo amani na utulivu nchini vitaendelea kudumishwa kwa kuwa kuvunjika kwa amani kuna athari kwa wananchi wote.

“Ukidanganywa ukachoma shule, atakayekosa elimu ni mtoto wako, ukichoma zahanati bado athari itakuwa kwako wewe mwenyewe, niwaaombe tulinde amani yetu kwa wivu mkubwa na ninawaahidi, ndani ya muda mfupi ujao maisha yetu katika wilaya hii yatabadilika sana kwa akuwa Serikali ina mipango mizuri kwaajili yenu,” amesema

Amesema chama hicho kimebaini kuwa hitaji kubwa la wananchi ni maendeleo na ndio maana kiko mstari wa mbele katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa ukubwa ili kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto za kimaendeleo zinazowakabili wananchi.

Akiwa katika kikao hicho, Kihongosi pia amewezesha upatikanaji kwa Sh300,000 kwa ajili ya ununuzi wa viti ili kuboresha shughuli za utendaji katika shina hilo namba 12.

Katika hatua nyingine, Kihongosi amekagua maendeleo ya mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa wilayani Geita kwa thamani ya zaidi ya Sh124 bilioni.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi Geita, Frank Changawa amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa Aprili 2025 umefika asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.

“Mradi ukikamilika tutakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 45 za maji wakati kwa sasa tunazalisha lita milioni 8 na mahitaji ni lita 22 milioni, hivyo ukikamilika tutazalisha ziada kwa wilaya nzima Geita,” amesema.

Akizungumzia mradi huo, Kihongosi amesema ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2025/30 ambapo pamoja na mambo mengine upatikanaji wa maji unatarajiwa kufika asilimia 95 kwa maeneo ya mijini na asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini.

“Huu mradi ukikamilika tutavuka malengo hayo na hii ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM, tunaomba mtuamini tukisema CCM ndio kinara wa maendeleo tunamaanisha,” amesema Kihongosi.