Madeleka: Wananchi waache kujichukulia sheria mkononi

Arusha. Wakati Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha likiendelea kuwasaka wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya askari Polisi, Roland Mollel, Wakili Peter Madeleka ameonya hali hiyo akisema hakuna mtu anayeruhusiwa kujichukulia sheria mkononi.

Amesema vyombo vya dola vinawajibika kuchukua hatua stahiki za kuwatafuta waliofanya tukio hilo na kuwafikisha katika mkono wa sheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Aprili 16, 2026 na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo, mauaji hayo yalitokea usiku wa Aprili 15, 2026 katika Mtaa wa Mlimani, Kata ya Muriet.

Akizungumza na Mwananchi, Wakili Madeleka amesema kitendo kilichofanywa na wananchi hakiwezi kukubalika katika jamii inayozingatia haki, akibainisha kuwa kosa la kuua ni la jinai na ni kinyume na haki za binadamu.

“Kitendo hicho kinasikitisha na ni muhimu wananchi kukumbuka kwamba nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Hakuna mtu anayeruhusiwa kujichukulia sheria mkononi. Kitendo cha kumuua mtu mwingine ni kosa kwa mujibu wa sheria zetu.

“Ninaamini vyombo vinavyohusika vitachukua hatua stahiki kuwatafuta waliofanya tukio hilo la kihalifu, kuwakamata na kuwafikisha katika mkono wa sheria. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema mtu yeyote anahesabika hana hatia hadi atakapothibitishwa na mahakama.

“Kama kuna mtu anatuhumiwa kwa kosa lolote, iwe wizi wa bodaboda au kosa lingine, anatakiwa kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria ili apate haki,” amesema Madeleka.

Ili kukomesha vitendo hivyo katika jamii, amesema elimu ya uraia inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi.

“Ni ukosefu wa ufahamu wa kisheria. Kama unamtuhumu mtu, wajibu wako kama mwananchi ni kwenda kutoa taarifa polisi ambao wana mamlaka ya kukamata, kuchunguza na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani. Hakuna sheria inayoruhusu mwananchi kumuua mwingine kwa kisingizio chochote,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani, Yohana Gasper, amesema inadaiwa askari huyo alikuwa akitekeleza jukumu la kukamata pikipiki zenye changamoto za taa. Wakati akiwa anauliza maswali, wananchi katika eneo la Tanzanite walimzingira na kuanza kumkimbiza.

“Inadaiwa alijitambulisha ni askari, lakini alipodaiwa kitambulisho, watu walikuwa wengi eneo hilo. Kutokana na hali hiyo, alijaribu kukimbia na wananchi wakaanza kumkimbiza.

“Inasemekana walipofika eneo la Tanzanite, pikipiki ilianguka ndipo tatizo likaanza. Inadaiwa walikuwa wawili, lakini haijajulikana kama mwenzake alikuwa askari au bodaboda. Ndipo walipomshambulia hadi kufariki dunia,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuepuka kuchukua sheria mkononi, akisisitiza kuwa hata kama mtu anahisiwa kuwa mwizi, anapaswa kupelekwa kituo cha polisi.

“Watu wanasema mambo mengi, lakini naamini uchunguzi unaendelea na chanzo cha tukio kitajulikana,” amesema.

Kamanda Masejo amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Roland alikuwa akiendelea na shughuli zake binafsi baada ya kazi, ndipo kulipotokea taharuki iliyosababishwa na taarifa za uwepo wa watu wanaodaiwa kuwa wezi.

Amesema wakati hayo yakiendelea, Roland akiwa amepanda pikipiki pamoja na mtu mwingine anayedaiwa kuwa dereva bodaboda, kundi la watu lilianza kuwashambulia huku likiwakimbiza.

“Msako bado unaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika, pamoja na kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo,” amesema Kamanda Masejo na kuongeza:

“Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaoendekeza tabia ya kuchukua sheria mkononi kwa kuongozwa na hisia, kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kusababisha madhara kwa watu wasio na hatia.”

Familia ya marehemu haijawa tayari kuzungumza na waandishi wa habari kufuatia msiba huo.

Huyu ni askari wa pili ndani kuuawa ndani ya miezi sita, baada ya Oktoba 11, 2025, askari Omary Mnandi (30) kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani, baada ya kudhaniwa kuwa mwizi.

Tukio hilo lilitokea katika baa ya Simaloi, iliyopo eneo la Kalolebi, ambapo ilidaiwa kuwa Mnandi aliingia kwenye gari lisilo lake na kulala ndani, hali iliyosababisha kushambuliwa na wananchi waliodhani ni mwizi.