Miti 500 yapandwa Olmoti Sekondari kukabili mabadiliko tabianchi

Arusha. Zaidi ya miti 500 imepandwa katika Shule ya Sekondari Olmoti iliyopo Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, kuendeleza kampeni ya Serikali ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika Shule ya Sekondari Olmoti, jumla ya miti 500 imepandwa, ambapo 200 ni miti ya vivuli na 300 ni miti ya matunda, iliyosambazwa katika maeneo mbalimbali ya shule hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi miti hiyo kwa uongozi wa shule, meneja mauzo wa Kampuni ya vinywaji ya Bonitte botlers Ltd, Joseph Simplis amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za utunzaji wa mazingira na kuunga mkono juhudi za serikali za kurejesha uoto wa asili.

“Miti hii itasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi kwa kuwapatia maeneo yenye kivuli kwa ajili ya kujisomea wakati wa muda wao wa ziada.

“Aidha, miti ya matunda itachangia lishe bora mara itakapoanza kuzaa,” amesema.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Olmoti wakishiriki kupanda miti waliyopewa na Kampuni ya Bonite Bottlers Ltd, katika jitihada za kukuza utunzaji wa mazingira shuleni hapo.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Martha Lwiva, amesema wameamua kuwashirikisha moja kwa moja wanafunzi katika shughuli hiyo ili kuwajengea moyo wa umiliki na uwajibikaji.

Ameeleza kuwa kila mwanafunzi kutoka kidato cha kwanza hadi cha tatu atapewa mti wa kupanda na kuutunza kama sehemu ya kumbukumbu na wajibu wa mazingira.

“Shule yetu ina zaidi ya wanafunzi 1,400, lakini tumeamua kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha tatu apande na kutunza mti wake. Hii itawajengea nidhamu na kumbukumbu nzuri kwao,” amesema Lwiva.

Mwanafunzi wa kidato cha pili, Francis Aloyce, amesema wamefurahia kupatiwa miti ya matunda ambayo itasaidia kuboresha lishe shuleni.

Amesema pia miti ya vivuli itawawezesha kupata mazingira mazuri ya kujisomea kwa utulivu.