Dar es Salaam. Wabunge wametaka njia rahisi ya upataji mikopo kwa vijana ikiwemo unafuu wa masharti, dhamana, usimamizi, kutokuundwa kwa vikundi pamoja na utolewaji wa elimu.
Hivi karibuni, Serikali ilitoa Sh200 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa vijana na wanawake kupitia ombi la mtu mmoja au kikundi wakiwa na andiko la mradi au biashara, huku lengo likiwa ni kujiendeleza kiuchumi.
Leo Jumatatu, Aprili 20, 2026, bungeni jijini Dodoma, wabunge wakichangia bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka kwa mwaka wa fedha 2026/27 ya Sh35 bilioni wameonesha wasiwasi wa fedha hizo kukwama benki endapo hatua zisipochukuliwa mapema.
Mbunge wa Ngara (CCM), Doto Bahemu licha ya kupongeza jitihada zinazofanywa na Waziri Nanauka na kuanzishwa kwa wizara hiyo na kusikiliza vijana, lakini haoni kama tatizo la ajira linaweza kumalizika haraka.
Bahemu amesema changamoto nyingi zinazowahusu vijana mwisho wa siku kinachohitajika ni fedha na inapatikana katika maeneo mbalimbali ikiwemo ajira na mipango yote tukipanga pasi na fedha haina tija.
Kuhusu Sh200 bilioni, Bahemu ameungana na wabunge wengine akisema kabla benki ya vijana haijaanzishwa hizo fedha zinakwenda tofauti: “Sisi vijana tulivyotarajia, hatujui huko zimekwenda kiasi gani.”
Mbunge Ndanda (CCM), Faraji Nandala amesema bado kuna malalamiko mengi kwa vijana hasa urasimu unaotokana na kitendo cha fedha hizo kupelekwa wizara nyingine za kisekta.
“Vijana wanalalamika hizi fedha kwanza hawana taarifa na hawajui mchakato mzima wa kuzipata fedha hizo. Idadi ya vijana walioomba hadi sasa ni 30,383 na ukiangalia waliolengwa ni vijana milioni 21 sasa idadi ya walioomba haifiki hata asilimia moja ya walengwa,” amesema.
Amesema Serikali kama inataka kuwasaidia vijana ifanye mapitio upya pia ipunguze masharti kama kuwa na TIN namba (cheti cha utambulisho wa mlipa kodi), leseni huku akitolea mfano vijana wa vijijini ambao si rahisi kuwa nazo.
“Hizi fedha zingegawanywa kwa majimbo kisha kata ambapo zingeshuka hadi ngazi ya kijiji ili vijana wapate na sio kuwa wizarani kama ilivyo sasa,” amesema.
Kuhusu fedha hizo kugawanywa wizara za kisekta, Mbunge la Kalambo, Edefonce Kanoni amesema zinapaswa kuwepo katika wizara yao ya vijana.
“Fedha hizi zirudi Wizara ya Vijana ili wawe wanajua kwamba zipo kwenye wizara yao kwa sasa zipo kilimo, uvuvi zinapaswa kurudi ili waziri azisimamie mwenyewe,” amesema.
Pia, mbunge huyo amesema masharti kuwa mengi yanakwamisha akihoji kijana kuambiwa aoneshe biashara walioanzisha na ametoka chuo kikuu anaitoa wapi.
“Wakienda benki wanakutana na masharti mengi hii inasababisha fedha hizi kukwama benki sasa zikibaki huko ni kwa manufaa ya nani?
“Sheria, usimamizi ubadilishwe na masharti yawe nafuu kama ni dhamana wabunge tupo, madiwani wapo na wenyeviti wapo masharti yapunguzwe vijana wapate fedha hizo,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Juakali amesema kitendo cha fedha kupelekwa katika wizara za kisekta kama kilimo, uvuvi, madini na michezo kunaleta maswali nani msimamizi wa fedha hizo?
“Kwenye wizara hizo aulizwe nani? Tunatakiwa kuanzisha mfumo maalumu wa kuwasaidia ikiwemo kupata elimu. Sio vijana wote wanaweza kuandika maandiko bado kuna haja ya kuwasaidia kwa sababu nafasi na muda upo,” amesema.
Mbunge huyo amesema vijana wawezeshwe kwenye kilimo cha kisasa, ujasiriamali, kurasimisha sekta zisizo rasmi kuwa rasmi na elimu ya ujuzi wa kisasa.
Mbunge wa Kasulu Vijijini, Edibily Kinyoma ameshauri mifuko na fedha zote zinazohusu maendeleo ya vijana ziwe katika Wizara ya Vijana kwa kuwa italeta urahisi hata kwa waziri kusema fedha zimefanyiwa nini pale atakapoulizwa.
Benki ya Maendeleo ya vijana
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Abdallah Issa amesema ipo haja ya kuwa na benki ya maendeleo ya vijana kwa sababu asilimia 76 ya nguvu kazi ya nchi ni vijana.
“Vijana wanatakiwa kupata fursa ya mitaji kupitia benki hiyo, kama tumeweza kuwa na benki ya maendeleo ya kilimo kwa nini tushindwe ya vijana,” amehoji.
Zainab anasema leo hii kuna programu na mifuko 74 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi lakini pengine vijana wanaweza wakawa wanafahamu mifuko miwili tu wa asilimia 10 na mfuko wa maendeleo ya vijana.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ilemela, William Kafiti, ameomba Serikali iendelee kutoa fedha katika vyuo vya maendeleo ya vijana vilivyopo Morogoro na Songwe ili waendelee kunufaika hasa katika maeneo ya ujasiriamali na kilimo.
Mbunge huyo amesema mpango kama wa (Building a Better Tomorrow) kuendelea kuweka msisitizo ili vijana wanaomaliza mikataba Jeshi la Kujenga Taifa na vyuo waanzishiwe mashamba wakalime.
