Monduli. Zaidi ya wakazi 10,000 katika Wilaya ya Monduli watanufaika na ugawaji wa matenki 500 ya kuhifadhia maji, kila moja likiwa na uwezo wa lita 5,000, ikiwa ni sehemu ya mradi wa uvunaji wa maji ya mvua unaolenga kupunguza uhaba wa maji hasa kipindi cha ukame.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Kijiji cha Losimingori, Mratibu wa mradi huo, Mbayani Tayai, amesema pia unahamasisha jamii kuona umuhimu wa kuvuna maji ya mvua ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji.
Amesema ugawaji huo umeenda sambamba na mbio za kilomita tano za nyika maarufu kama Run with the Maasai, zilizowashirikisha zaidi ya watu 400, kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu matumizi bora ya rasilimali maji.
Tayai amesema mradi huo wenye thamani ya Sh500 milioni umewezeshwa na kundi la vijana maarufu wa mitandao ya kijamii kutoka Marekani, waliokusanya fedha kupitia kampeni mbalimbali za mtandaoni.
“Hawa ni vijana wenye ushawishi mkubwa mitandaoni ambao wameamua kuelekeza sehemu ya mapato yao kusaidia jamii za Kimasai katika Wilaya ya Monduli kupitia mradi huu wa maji,” amesema.
Ameongeza kuwa uvunaji wa maji ya mvua unaweza kuwa suluhisho la kudumu kwa tatizo la maji nchini iwapo utawekewa mkazo, huku ukichangia pia kupunguza mzigo kwa wanawake na wasichana wanaotumia muda mwingi kutafuta maji.
Kwa mujibu wa Tayai, mpango huo unalenga kufikia vijiji vyote katika kata 20 za Wilaya ya Monduli zenye takribani kaya 60,000 na wakazi wapatao 300,000, huku mipango ikiendelea ya kusambaza matenki kwa kaya nyingine 55,000 katika siku zijazo.
Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonyesha kuwa Tanzania ina takribani kaya milioni 14, idadi inayotarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya majengo ya makazi milioni 15 ifikapo mwaka 2026. Inakadiriwa pia kuwa paa lenye ukubwa wa mita za mraba 190 linaweza kuvuna hadi lita 180,000 za maji kwa mwaka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Kisioki Moitiko, amesema mbali na mradi wa matenki kwa kaya, halmashauri hiyo imeanza kujenga miundombinu ya umma ikiwamo visima na mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, amesema mradi huo ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa katika maeneo mengine ya jamii za wafugaji zinazokabiliwa na changamoto ya maji.
Naye Mbunge wa Monduli, Isaac Joseph Copriano maarufu ‘Kadogoo’, amewataka wananchi kutunza matenki hayo ili yaweze kudumu na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
