Kibaha. Wananchi wa kata za Tangini, Pangani na Kidimu katika Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani wameeleza faraja yao kufuatia kusogezewa huduma za afya kupitia Zahanati ya Tangini, wakisema hatua hiyo inapunguza gharama, muda wa kusaka huduma na vifo vinavyoweza kuzuilika.
Zahanati hiyo iliyojengwa kwa gharama ya Sh234 milioni imeanza kutoa huduma, huku ikiwanufaisha wakazi wa maeneo hayo ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
Akizungumza leo Jumatatu, Aprili 20, 2026 Mkazi wa Tangini, Aneth Maxwell, amesema kabla ya uwepo wa zahanati hiyo walikuwa wakipata usumbufu mkubwa kufuata huduma za afya mbali na makazi yao.
“Nimehudumiwa vizuri bila usumbufu wowote. Tunaishukuru Serikali kwa kutusogezea huduma hizi muhimu karibu yetu,” amesema.
Naye mkazi mwingine, Rukia Mahenge, amesema awali alikuwa akitumia kati ya Sh6,000 hadi Sh8,000 kwa usafiri wa kwenda na kurudi kutafuta huduma za afya kulingana na msimu.
“Wakati wa jua nilikuwa natumia Sh6,000, na wakati wa mvua Sh8,000. Sasa tunaweza kufika kwa kutembea au kutumia hata Sh1,000 tu. Hii ni faraja kubwa kwetu,” amesema.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Tangini, Lazaro Benjamin, amewataka wahudumu wa afya kuhakikisha wanatoa huduma bora ili zahanati hiyo ilete tija iliyokusudiwa.
Amesema pia ni wajibu wa wananchi kuilinda miundombinu hiyo ili iendelee kuhudumia jamii kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Baraka Makaya, amesema pamoja na gharama za ujenzi, zahanati hiyo imepokea vifaa tiba vyenye thamani ya Sh50 milioni.
Amesema tayari huduma muhimu zimeanza kutolewa.
“Zahanati hii itahudumia wakazi wa kata tatu za Tangini, Pangani na Kidimu. Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati,” amesema.