Simiyu. Wakati gharama za nishati ya kupikia zikiendelea kuwa mzigo kwa wananchi wengi vijijini, ujio wa majiko banifu 1,247 wilayani Maswa umeibua matumaini mapya ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuokoa muda na kulinda mazingira.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imepokea majiko hayo ya kutumia mkaa, yakilenga kutoa suluhisho la haraka kwa changamoto ya nishati ya kupikia, inayochangia uharibifu wa misitu na athari za kiafya kwa watumiaji.
Akizungumza leo, Aprili 16, 2026, wakati wa mapokezi ya majiko hayo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Maisha Mtipa, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi, hususan wa kipato cha chini.
“Majiko haya ni suluhisho la haraka kwa changamoto ya nishati ya kupikia. Tunatarajia kuona kupungua kwa matumizi ya kuni, ukataji miti holela na kuboreshwa kwa afya za wananchi wetu,” amesema Mtipa.
Meneja Usambazaji wa Majiko Banifu wa Kampuni ya Geita Millenium Star Ltd, Khamis Yahaya akitoa maelezo kwa wananchi wa wilaya ya Maswa jinsi ya kutumia jiko hilo. Picha na Samwel Mwanga
Ameongeza kuwa halmashauri imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha majiko hayo yanawafikia walengwa waliokusudiwa, huku ufuatiliaji ukifanyika ili kuhakikisha matumizi yake yanaleta matokeo chanya.
Majiko hayo yametolewa kupitia mradi wa usambazaji unaotekelezwa na kampuni ya Geita Millennium Star Ltd, ukiwa na lengo la kunufaisha mamia ya kaya kwa kupunguza gharama za upishi na muda unaotumika kutafuta kuni, mzigo unaowaathiri zaidi wanawake na watoto.
Hata hivyo, Mtipa amebainisha kuwa mahitaji bado ni makubwa, akieleza kuwa wilaya hiyo ina wakazi takribani 426,000, wengi wao wakitegemea kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia.
Kwa upande wake, meneja usambazaji wa kampuni hiyo, Khamis Yahaya, amesema gharama halisi ya jiko moja ni Sh41,000, lakini kutokana na ruzuku ya Serikali, wananchi watalipia Sh5,250 pekee.
Sehemu ya wananchi wa wilaya ya Maswa waliojitokeza katika zoezi la ugawaji wa majiko banifu ya kutumia mkaa kidogo. Picha na Samwel Mwanga
“Lengo ni kupunguza uharibifu wa mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hasa kwa wananchi wa kipato cha chini,” amesema Yahaya.
Mkazi wa Kitongoji cha Sola, Isack Maduhu, amesema majiko hayo yatapunguza muda unaotumika kutafuta kuni na kutoa nafasi kwa shughuli nyingine za maendeleo.
“Tunatumia muda mwingi porini kutafuta kuni. Majiko haya yatatusaidia na kutupa muda wa kufanya mambo mengine ya maendeleo,” amesema.
Naye Juliana John, mkazi wa Kata ya Shanwa, amesema kupanda kwa bei ya mkaa kumekuwa changamoto, hivyo matumizi ya majiko banifu yatasaidia kupunguza gharama za maisha.
Kwa upande wake, Rehema Joseph, mama lishe mjini Maswa, amesema changamoto ya moshi imekuwa ikihatarisha afya zao, hivyo matumaini yao ni kuona mazingira bora zaidi ya upishi.
“Moshi unatuchosha na kuathiri afya. Kama majiko haya yanapunguza moshi, yatatusaidia kufanya kazi vizuri zaidi,” amesema Rehema.
