CCM yaikaribisha Chadema ulingoni, kushindana kwa hoja na sera

Geita. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefurahishwa na uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufaa kukirudisha kwenye ulingo wa siasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Chama hicho tawala kimesema kiko tayari kukabiliana na Chadema kwa hoja na sera katika majukwaa mbalimbali ya kisiasa nchini.

CCM kimetoa kauli hiyo siku moja baada ya Mahakama ya Rufaa kutoa hukumu iliyobatilisha zuio la kutokufanya shughuli za kisiasa kwa Chadema lililotolewa na Mahakama Kuu, kufuatia kesi ya madai ya mgawanyo wa rasilimali za chama baina ya Bara na Zanzibar.

Pia, Mahakama ya Rufani imeelekeza kesi ya msingi iendelee kusikilizwa na jaji mwingine ambaye atatakiwa kuchunguza na kujiridhisha iwapo ilifunguliwa ndani ya muda au la kabla ya kuendelea na hatua nyingine.  Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa Jaji Hamidu Mwanga.

Hukumu hiyo ilitolewa jana Jumatano, Aprili 15, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani: Augustine Mwarija, Issa Maige na Abraham Mwampashi.

Kutokana na uamuzi huo, Chadema ambacho kilikuwa kifungoni kwa siku 309, kuanzia Juni 10, 2025 tayari kimetangaza kuitisha kamati kuu Aprili 28 na 29 itakayofanyika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam, huku kikisisitiza kitaendelea kuwapigania wananchi.

Viongozi wa Chadema wakiwa katika Makao Makuu ya chama hicho leo Jumatano Aprili 15, 2026, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Leo Alhamisi, Aprili 16, 2026, akizungumza kwa nyakati tofauti wilayani na mkoani Geita Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amesema uamuzi huo ni kielelezo Serikali ya CCM imeviacha vyombo vya uamuzi ikiwemo Mahakama kufanya majukumu yake kwa uhuru bila kuingiliwa.

“Nimefurahi kusikia Chadema wameruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa, walishtakiana wao kwa wao kisa ugomvi wa mali, Waswahili wanasema ndugu wakigombana chukua jembe kalime, Mahakama imetoa uamuzi sasa tunawasubiri kwenye majukwaa,” amesema.

Amesema chama hicho kitaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya uamuzi na hakitaingilia shughuli zao ili viweze kufanya kazi kwa weledi kuhakikisha vyombo hivyo vinakuwa huru na kutoa haki kwa pande zote bila upendeleo.

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walivyowasili makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo Jumatano Aprili 15, 2026. Picha na Michael Matemanga

Amesema viongozi wa Chadema wanapaswa kutambua juhudi za Serikali katika kuimarisha utawala wa sheria na misingi ya haki nchini bila ubaguzi wowote.

Kihongosi amesema amemsikia Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, John Heche akitangaza chama hicho kufanya ziara nchi nzima jambo ambalo amesema ni vema, kwani watakutana kwa wananchi kupitia majukwaa ya kisiasa kunadi sera na hoja za vyama vyao.

Amesema CCM inakubalika na kuaminika na wananchi jambo ambalo ameeleza ndio siri ya ushindi wa chama hicho katika chaguzi mbalimbali, na chama hicho kitaendelea kushindana kisiasa kwa hoja na sera.

“Kuna watu huwa wanahoji CCM tunashindaje kwenye chaguzi, jibu liko wazi sisi tuna watu kuanzia ngazi ya shina yaliyopo nchi nzima wakati wenzetu hawana utaratibu huo, wakati wa kugombea wanakuja na watu ambao baada ya kumalizika kwa uchaguzi wanaondoka sasa unategemea nini kama sio CCM kuendelea kushinda,” amesema.

Wakizungumza kuhusu Chadema kuruhusiwa kuendelea na shughuli za kisiasa baadhi ya wakazi wa Katoro wamesema uamuzi huo ni wa busara na utasaidia kukuza demokrasia nchini.

John Lutubija amesema kutolewa kwa uwanja huru kwa vyama vyote vya siasa ni njia nzuri ya kuwaruhusu wananchi kusikiliza sera na hoja za vyama vyote na kisha kufanya maamuzi kwa masilahi ya jamii kwa ujumla.

“Uamuzi ni mzuri na utasaidia wananchi kuwa na uwanja mpana wa kupima na kuona chama kipi kina nia njema na Watanzania kisha watakiunga mkono,” amesema

Maduka Emmanuel amesema Watanzania wanahitaji utulivu na amani hivyo vyama vyote vya siasa vinatakiwa kuhakikisha vinazingatia suala hilo, na kamwe wananchi wasikubali kuunga mkono chama chochote kitakachokuwa na nia ya kuleta vurugu.

“Vyama vyote viko huru kufanya siasa lakini vizingatie amani, na utulivu wa nchi, sote tumeshuhudia yaliyotokea Oktoba 29,2025 Watanzania kwa pamoja tusikubali kushuhudia hali ile tena hapa nchini kwetu,” amesema.

Neema Sahani amesema vyama vya siasa visitumike kuvunja misingi imara ya nchi iliyowekwa na waasisi.

“Suala la upendo, umoja, mshikamano, kuvumiliana ni masuala muhimu hayana itikadi za chama hivyo vyama vyote vinatakiwa kuzingatia mambo hayo,” amesema.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Mji wa Katoro, Kihongosi amesema Serikali ya CCM bado ina dhamira ya dhati kutekeleza ahadi zote zilizoahidiwa wakati wa kampeni hivyo kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM,Kenani Kihongosi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kakubilo wilayani Geita mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Geita.

Amesema tayari Serikali imeanza kutekeleza ahadi hizo ikiwamo utekelezaji wa miradi ya maji ili kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji nchini unapata suluhisho la kudumu.

Ametolea mfano wa utekelezaji wa mradi wa maji Geita wenye thamani ya Sh124 bilioni ambao ukikamilika utamaliza kabisa tatizo la ukosefu wa maji katika Wilaya ya Geita na baadhi ya maeneo ndani ya Mkoa wa Geita.

“Hapa Katoro kulikuwa na shida ya moto, vibanda vya biashara vilikuwa vikiungua moto mara kwa mara na hamkuwa na gari la zimamoto lakini Serikali yenu tayari imeleta gari la Zimamoto kukabiliana na hali hiyo, pia suala la changamoto ya barabara tayari imewekewa mipango madhubuti hivyo niwathibitishie Katoro hii itakuwa bora zaidi muda mchache ujao,” amesema.

Amesema kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa katika eneo hilo la Katoro ambapo wastani wa watoto 1,000 huzaliwa kila mwezi, Serikali tayari imejenga hospitali ili kuhakikisha hakuna anayepoteza maisha wakati wa kujifungua huku watoto pia wakizaliwa salama.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kakubilo wilayani Geita mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo.

Kihongosi amesema ahadi zote zilizotolewa na chama hicho zitatekelezwa zote utekelezaji ambao utafanyika kwa awamu kutokana na ukweli kuwa maendeleo ni mchakato na Watanzania wanatakiwa kuendelea kuwa na imani na chama hicho, kwani kina nia madhubuti ya kuwatumikia.

Kihongosi pia amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Geita kushughulikia changamoto ya mikopo umiza maarufu kama kausha damu kwa maelezo kuwa CCM haipo tayari kuona watu wake wananyanyaswa na baadhi ya watu.