Aliyekutwa na kucha, meno ya Simba akwaa kisiki mahakamani

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga, imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na Zahoro Masala aliyekuwa akipinga kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na nyara za Serikali.

Mahakama imeridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi bila shaka yoyote, huku hoja zote tano za rufaa zikikosa msingi wa kisheria.

Hukumu hiyo iliyotupilia rufaa hiyo imetolewa na Jaji Abubakar Mrisha, Aprili 14, 2026, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji Mrisha amesema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulikuwa wa kuaminika na wa kutosha kumtia hatiani mrufani.
 

Zahoro alifikishwa mahakamani pamoja na washtakiwa wenzake wawili kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi, yakiwemo kumiliki na kufanya biashara haramu ya nyara za Serikali.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi,shtaka la kwanza ilidaiwa Mei 8, 2017 katika Kijiji cha Uzega wilayani Mlele,Katavi walikutwa na kucha mbili za simba na meno 16 ya simba kinyume cha sheria, yaliyokuwa na thamani ya Dola za Marekani 19,600 sawa na Sh43.3 milioni.

Hata hivyo, mahakama ya mwanzo iliwaachia huru katika shtaka la pili na la tatu kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha, huku Zahoro pekee akikutwa na hatia katika shtaka la kwanza la kumiliki nyara hizo kinyume cha sheria.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita na vielelezo mbalimbali ikiwemo nyara zenyewe, huku mrufani akijitetea peke yake bila kuwasilisha ushahidi wa ziada.

Baada ya kusikiliza pande zote, mahakama ya mwanzo ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela.

Akiwa hajaridhika na uamuzi huo, Zahoro aliwasilisha rufaa Mahakama Kuu akiwa na sababu tano ikiwemo madai kuwa shtaka halikuthibitishwa bila shaka, kulikuwa na mapungufu katika mnyororo wa ulinzi wa vielelezo, mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, pamoja na kutokuwepo kwa shahidi huru wakati wa upekuzi.
 

Uamuzi Mahakama

Katika uchambuzi wake, Jaji Mrisha alieleza kuwa msingi wa kwanza wa rufaa, uliodai kuwa shtaka halikuthibitishwa, hauna uzito na kuwa ushahidi hasa wa shahidi wa kwanza, pili na sita uliungana vizuri na kuthibitisha kuwa mrufani alipatikana na nyara hizo kinyume cha sheria.

Kuhusu hoja ya mnyororo wa ulinzi wa vielelezo, mahakama ilibaini kuwa kulikuwa na rekodi sahihi ya namna ushahidi ulivyohifadhiwa na kuhamishwa kutoka kwa maofisa mmoja hadi mwingine bila kuchezewa.

Jaji Mrisha alisisitiza kuwa mnyororo huo ulikidhi matakwa ya kisheria na haukuvunjika kama ilivyodaiwa na mrufani na kuwa wakati mahakama inasikiliza kesi hiyo cheti cha ridhaa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, kilikuwepo na kilikubaliwa kabla ya kuanza kwa kesi, hivyo kuondoa hoja hiyo kabisa.

Kuhusu malalamiko ya kutokuwepo kwa shahidi huru wakati wa upekuzi, mahakama ilikiri kuwa ingekuwa vyema shahidi wa aina hiyo kuwepo, lakini ikasisitiza kuwa mazingira ya tukio yaliyofanyika msituni yalifanya iwe vigumu kumpata shahidi huru.

Aidha imesema uwepo wa sahihi ya mrufani katika cheti cha kukamatwa ulithibitisha kuwa alikamatwa na nyara hizo.

Katika hoja ya mwisho, iliyodai kuwa mahakama ya mwanzo haikuzingatia utetezi wa mrufani, Jaji Mrisha alikubaliana kwa sehemu kuwa baadhi ya maelezo hayakuzingatiwa kikamilifu.

Aidha alieleza kuwa hata kama yangepatiwa uzito, yasingebadilisha matokeo ya kesi kutokana na uzito wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

“Kwa ujumla, ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulikuwa thabiti na wa kuaminika kiasi cha kuthibitisha hatia ya mrufani bila shaka yoyote,” alieleza jaji katika hukumu yake.

Kutokana na uchambuzi huo, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa hoja zote tano za rufaa hazina msingi, na hivyo kuitupilia mbali rufaa hiyo.