IGP Wambura aeleza maboresho vituo vya afya vya polisi

Morogoro. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura amesema vituo vya afya vya polisi vitaendelea kuboreshwa katika eneo la miundombinu, vifaa tiba na kuwekeza katika rasilimali watu ikiwemo kuajiri wataalamu wapya wa afya, ili vituo hivyo viweze kutoa huduma bora kwa askari na jamii inayozunguka vituo hivyo.

IGP Wambura ameyasema hayo leo Aprili 16,2026 mkoani Morogoro wakati akifungua mkutano wa wakuu wa vituo tiba, wahasibu na watendaji wa kikosi cha afya nchini.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuboresha matumizi ya Tehama hivyo amewataka watoa huduma kuwa wepesi katika kujifunza na kutumia mifumo iliyopo ili kutoa huduma bora kwa wateja wa ndani na nje wanaopata huduma katika zahanati na vituo vya afya vya Polisi.

Aidha, amewataka watendaji wa kikosi cha afya kufanya tathmini ya magonjwa mbalimbali ili kujua hatua za kuchukua katika kuboresha afya za askari na familia zao, ikiwemo kusaidia kamisheni ya polisi jamii katika kuwafikia wananchi ili kutimiza lengo la Jeshi la Polisi ambalo ni kuzuia uhalifu kabla haujatokea.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Afya, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya ameeleza kuwa kikao hicho kinalenga kufanya tathmini ya huduma zinazotolewa na kikosi hicho ambapo amesema kwa sasa wamejipanga kwenda kutumia mifumo ya Tehama ili kuboresha huduma zaidi zinazotolewa kwenye zahanati na vituo vya afya vya Polisi, baada ya kupatiwa fedha na Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kazi hiyo.

Amesema katika uongozi wa IGP Wambura kumekuwepo na mafanikio mbalimbali ikiwemo maboresho ya majengo na vifaatiba jambo linaloboresha huduma kwenye hospitali na zahanati hizo.

Wakuu wa vituo tiba, wahasibu na watendaji wa kikosi cha afya Cha jeshi la polisi nchini wakimsikiliza mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Camillus Wambura alipokuwa akifungua mkutano maafisa hao uliolenga kujadili maboresho ya vituo vya afya vya polisi na utendajikazi wa vituo hivyo. Mkutano huo umefanyika mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff

Aidha, amesema wanaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa askari polisi na wananchi wanapata huduma bora.

Kwa upande wake Mkuu wa Utawala ndani ya Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, Anthony Ruta amesema huduma bora za afya kwa askari na familia zao ni nguzo muhimu katika ufanisi wa kazi za polisi.