Barker ashtukia kitu Simba, apangua kikosi chake

SIMBA imerejea nyumbani ikitokea Arusha ilikocheza mechi tatu ambazo mbili ni za ugenini za Ligi Kuu Bara na moja ikiwa kama mwenyeji wa Kombe la Shirikisho la CRDB, lakini inabadilisha njia tu ikiwafuata Namungo Jumamosi hii, huku kocha wa kikoso hicho, Steve Barker kuna kitu ameshtukia, hivyo ameamua kupangua mziki wake fasta.

Berker alichosema mbele ya Mwanaspoti ni kwamba, timu hiyo haiwezi kupata ubingwa na mastaa 11 tu wa kikosi cha kwanza na sasa atakuwa anapangua pangua mziki huo ili kutunza ubora wa mastaa wake kutokana na ugumu wa mechi za mashindano tofauti.

Amesema kwasasa atakuwa akifanya mabadiliko ya wachezaji wanaoingia kikosi cha kwanza kutokana na ratiba ngumu waliyonayo ya kumalizia msimu ili kuepuka kuporomosha viwango vya wachezaji wake.

“Msimu ni mgumu kama ambavyo unaona, huwezi kuchukua ubingwa kwa kutumia wachezaji 11 pekee ambao wanaanza mara kwa mara, unaweza kuwaumiza au kupungua ubora kutokana na uchovu, ratiba ya mechi zipo karibu karibu sana,” amesema Barker.

“Tunahitaji kutoa nafasi kwa wachezaji tofauti, tuna wachezaji wazuri kwenye timu yetu, kitu muhimu kwao ni kujipanga kwa kucheza na kushindania nafasi, kuna mashindani mengi ambayo aliye tayari atapata nafasi ya kuitumikia klabu.

“Unaweza kuona tumefanya mabadiliko na bado timu ilicheza vizuri mchezo wa jana (juzi) tukionyesha ubora mkubwa, tunajiandaa sasa kwenda kucheza mchezo mwingine wa ugenini dhidi ya Namungo na baada ya hapo tutakwenda kwenye mashindano mengine.”

Hesabu hizo za Barker zimeshaanza ambapo kwenye mchezo uliopita dhidi ya Fountain Gate aliwapumzisha nahodha wake na beki wa kulia, Shomari Kapombe, nafasi yake ikichukuliwa na David Kameta ‘Duchu’. Mwingine aliyepumzishwa ni Yusuf Kagoma, huku Clatous Chama ambaye alitokea benchi kwenye mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji, alianza mbele ya Fountain Gate na kufunga.

Mchezo huo dhidi ya Fountain Gate, pia Barker aliwapa nafasi kipindi cha pili Antony Mligo akimtoa Nickson Kibabage, beki kijana Hussein Mbegu aliyepandishwa timu kubwa akichukua nafasi ya Rushine De Reuck, wakati Morris Abraham akiingia akichukua nafasi ya Chama.

Simba ambayo itacheza na Namungo Aprili 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, ikimaliza mchezo huo itaelekea Zanzibar tayari kwa kuanza mashindano ya Kombe la Muungano, michuano itakayoanza Aprili 21 na kumalizika Aprili 29 mwaka huu.

Ikimaliza tu michuano hiyo ambayo pia Yanga, Azam na Singida Black Stars zinakwenda kushiriki kutokea Tanzania Bara, Simba itaikaribisha Yanga Mei 3, 2026 ikiwa ni duru la pili la Ligi Kuu Bara baada ya ile ya kwanza kumalizika kwa matokeo ya 0-0.