Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema Serikali imeanza mchakato wa kurasimisha sekta ya mamalishe na babalishe ili kuondoa changamoto za kiafya, kuboresha huduma na kuwafungulia fursa za kiuchumi.
Amesema kwa muda mrefu, mama na babalishe wamekuwa wakifanya kazi bila mwongozo maalumu, hali inayochangia kuwepo kwa hatari za kiafya kwa watumiaji wa huduma zao.
Dk Gwajima ametoa kauli hiyo jana Ijumaa Aprili 17, 2026 katika mahojiano maalumu kuelekea kongamano la mamalishe na babalishe nchini, linalotarajiwa kufanyika Aprili 21, mwaka huu, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema wameamua kuja na mpango huo kutokana na baadhi ya mamalishe na babalishe hawazingatii kanuni za msingi za usafi, jambo linaloweza kusababisha madhara kwa jamii.
“Tunayo mifano ya watu wanaandaa chakula bila kuzingatia usafi wa mazingira, afya binafsi au uhifadhi sahihi wa chakula. Hii inaweza kusababisha magonjwa kwa walaji,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imeamua kuweka mfumo rasmi wa kuwatambua na kuwaongoza ili kuhakikisha wanatoa huduma katika mazingira salama na yenye viwango vinavyokubalika.
Sehemu ya utekelezaji wa mpango huo, alisema ni kufanyika kwa kongamano hilo la kitaifa la mamalishe na babalishe huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Amesema kongamano hilo litawakutanisha wawakilishi kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kila mkoa utawakilishwa na mamalishe wanne viongozi wakisindikizwa na maofisa maendeleo ya jamii mmoja kila mkoa.
“Lengo ni kuwakutanisha ili tuwasikilize, tuwatambue rasmi na kuweka msingi wa namna bora ya kuwawezesha,” amesema.
Dk Gwajima amesema urasimishaji huo hautalenga kuwaongezea mzigo wa kodi, bali kuwawekea mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa usalama na ufanisi zaidi.
Amesema hatua ya kwanza itakuwa ni kuwasajili kidigitali mamalishe na babalishe wote nchini, ili kujua idadi yao, maeneo wanayofanyia kazi na changamoto wanazokutana nazo.
Kupitia mfumo huo, amesema kila mhudumu atakuwa na utambulisho utakaounganishwa na taarifa zake za Nida, jambo litakalorahisisha kuwafikia na kuwapatia huduma mbalimbali za maendeleo.
“Tunataka taarifa ziwafikie moja kwa moja. Wengi wao hawana muda wa kufuatilia vyombo vya habari kwa sababu muda mwingi wanakuwa kazini,” amesema.
Amesema kupitia usajili huo, wataunganishwa na fursa za mikopo nafuu, ikiwamo ile ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, pamoja na mikopo kutoka taasisi za fedha na kidogo inayotolewa na wizara yake.
Kwa sasa, amesema wengi wao hawafikiwi na fursa hizo kwa sababu hawajatambulika rasmi katika mifumo ya Serikali.
“Ukishakuwa kwenye mfumo, unakuwa sehemu ya wale wanaoweza kupata mikopo, mafunzo na taarifa nyingine muhimu za maendeleo,” amesema.
Kuhusu usafi, Dk Gwajima amesema Serikali itaweka miongozo ya msingi ya uendeshaji wa shughuli zao, ikiwamo viwango vya usafi, afya za wahudumu na ubora wa chakula kinachoandaliwa.
Amesema hatua hiyo inalenga kulinda afya ya walaji pamoja na wahudumu wenyewe, huku ikiimarisha imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa na kundi hilo.
“Tunataka mtu anapokula kwa mamalishe awe na uhakika wa usalama wa chakula anachokula,” amesema.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali inahamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa mamalishe na baba lishe ili kupunguza athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na matumizi ya kuni.
Dk Gwajima amesema ukweli ni kwamba sekta hiyo ni moja ya sekta zenye mchango mkubwa katika ajira na uchumi, hivyo haiwezi kuachwa nyuma katika jitihada za maendeleo ya Taifa.
Amesema kuelekea mwaka 2050, Serikali inalenga kuona sekta binafsi inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi, huku mamalishe na baba lishe wakisewa sehemu muhimu ya mnyororo huo.
“Tunataka kuona wanakua kutoka biashara ndogo hadi kuwa wamiliki wa migahawa mikubwa na kuchangia zaidi katika uchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa, kuna fursa pia katika utalii wa vyakula vya asili vinavyoweza kutumika kuvutia watalii ikiwa vitaboreshwa na kutangazwa ipasavyo.
Kupitia matumizi ya teknolojia, amesema itawezekana kwa watu kupata taarifa za maeneo ya mamalishe kwa urahisi, jambo litakalosaidia kuongeza wateja na mapato.
Akizungumzia uzoefu wake, Dk Gwajima amesema amewahi kukutana na mazingira yasiyoridhisha katika baadhi ya maeneo, hali iliyomfanya kuacha chakula licha ya kukilipia.
Amesema pia kuna maeneo yenye huduma bora na ladha ya kipekee, lakini wahudumu wake hawana uwezo wa kuwafikia wateja wengi kutokana na ukosefu wa mitaji na taarifa.
“Tunataka wale wanaofanya vizuri wapate nafasi ya kukua na kufikia masoko makubwa zaidi,” amesema.
Baada ya kongamano hilo, amesema Serikali itakaa pamoja na wawakilishi wa mama na baba lishe ili kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maazimio yatakayopatikana.
Mpango huo utaelekeza namna ya kutekeleza maelekezo ya Rais Samia na kuunganisha juhudi hizo na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050.
Dk Gwajima amesema pia kutakuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji, ikiwamo tathmini ya kila mwaka ili kupima mafanikio ya hatua hizo.
Amesisitiza kuwa, lengo ni kuleta mabadiliko ya kudumu katika sekta hiyo ili kuboresha huduma zao na kulinda afya ya jamii kwa jumla.
Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Umoja wa Mama na Baba Lishe (Umalita), Avijawa Omary amesema umoja huo ulinzia wilayani Kigamboni baada ya mwanachama mwenzao kufariki dunia na mtaa kususa kumzika kwa sababau haudhurii misiba ya watu wengine.
Akimtete, Avijawa amesema kutokana na kazi zao za kuamka asubuhi sana na kurudi usiku, jambo lililowafanya kufikiria kuanzisha umoja wao.
Avijawa amesema waliaanza na mamalishe 120, lakini moja ya jambo waliloibua licha ya kuwasaidia, ni kutokopesheka na taasisi za kifedha.
Amesema kadri siku zilivyokwenda walipungua hadi wakabaki watatu, lakini hawakukata tamaa wakaanza tena kutafuta wananchama na kufika 100.
Katika harakati za kutaka kusajili umoja huo, alisema walikutanishwa na Waziri Gwajima.
“Tunashukuru baada ya kukutana na waziri alitupa muongozo mzuri, tukajisajili na hivi sasa navyoongea tuna wanachama zaidi ya 5000 nchi nzima,” amesema Avijawa.
Akielezea matarajio yao katika kongamano hilo, Avijawa amesema ukiacha mbali kurasimisha rasmi, wanataka kukataa jina la kuitwa ‘Mama au Baba Ntitilie’ kwa kuwa linawafanya washindwe kujiamini na kushusha thamani yao.
“Kwenda kukutana na Rais wiki ijayo anakwenda kutuheshimisha kwa kuwa tangu Uhuru haijawahi kutokea, kwani tunaenda kubadili mtazamo kuhusu mama na baba lishe.
“Maana tunadili na mamalishe na babalishe hadi wa chini akiwamo anayechoma chapati na vitumbua barazani, tunahitaji miaka mitatu ijayo kundi hili nalo liwe katika kipato cha kati,” amesema.
Jingine wanalohitaji katika kundi hilo alisema ni kuwa na bima ya afya, kwa kuwa mamalishe au babalishe akipata ugonjwa wa kifua kikuu na kushindwa kujitibu, lazima atawaambukiza wateja wake.
“Kwa hiyo ukiwa na bima ya afya muda wowote ukisikia unaumwa utaweza kwenda hospitali kupata matibabu,” amesema.
Hata hivyo, amesema katika kongamano hilo wanaenda kubeba ajenda ya matumizi ya nishati safi, kwa kuwa wengi wameathirika na matumizi ya kuni akiwamo yeye.
Amesema wanataka kufika mahali kundi hilo wote wawe wanatumia nishati safi, kwani mbali kusaidia kutunza afya zao kutokana na moshi wa kwenye kuni au mkaa, pia wataweza kuchangia utunzaji wa mazingira.
Wakati Avijawa akisema hivyo, Tanzania inakabiliwa na janga la ukataji miti kwa kasi ya hekta 400,000 hadi 470,000 kwa mwaka, kunakochochewa uhitaji wa nishati ya mkaakuni, kilimo na ufugaji.
