Dodoma. Kamishna wa Elimu Tanzania, Dk Lyabwene Mtahabwa amesema mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji hauwezi kufanikiwa bila kuwepo kwa huduma bora za chakula na lishe shuleni.
Aidha, amewaagiza wadhibiti ubora kwenye halmashauri zote nchini kuhakikisha chakula wanachokula wanafunzi wanapokuwa shuleni kinaandaliwa kwa ubora wa hali ya juu ili kuwaepusha na madhara ya kiafya ikiwemo viriba tumbo.
Dk Mtahabwa ameyasema hayo Aprili 16, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuchochea mifumo imara, jumuishi na endelevu ya ununuzi wa chakula cha shule (CRISP), unaotekelezwa na shirika la kimataifa la SwissAid kwa kipindi cha miaka mitatu kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es salaam kwa thamani ya Sh1.9 bilioni.
Dk Mtahabwa amesema maboresho ya elimu hayawezi kuleta matokeo kama hayatazingatia lishe ya wanafunzi ndiyo maana Serikali imetunga sera na kutoa miongozo ili kuhakikisha kila shule inatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi.
“Mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji hatuwezi kufanikiwa bila kuwa na huduma bora za chakula na lishe. Kwa hiyo uboreshaji wowote ule wa elimu hatuwezi kufanikiwa kama hauko makini na uboreshaji wa huduma za chakula na lishe,” amesema Dk Mtahabwa.
Ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha lishe shuleni, ikiwemo waraka namba tatu wa mwaka 2006 uliolenga kushirikisha jamii katika utoaji wa huduma za chakula shuleni.
Amesema mwaka 2020, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa mwongozo wa utoaji wa huduma za chakula shuleni uliozinduliwa mwaka 2021 kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali zikiwemo Tamisemi, afya na kilimo.
Dk Mtahabwa amebainisha kuwa mwaka 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alisaini mkataba wa lishe na wakuu wa mikoa ili kuhakikisha huduma za chakula na lishe zinaboreshwa shuleni kote nchini.
Amesema mradi huu unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha elimu kwa kuwashirikisha wadau kwani sera ya elimu imelenga kumwimarisha mtoto kiakili, kimaadili na elimu ya kujitegemea.
“Tuwe makini na vyakula vya watoto wanavyonunua huko mashuleni ambavyo hatuna uhakika navyo ni muhimu kuangalia afya za watoto wetu kwa kuangalia vyakula wanavyopata huko ambavyo vina madhara kiafya baadaye,
Tusimkubali kwa vyovyote anayechezea afya za watoto wetu kwa hiyo nawaomba wenzetu wa Tamisemi, wadau wa elimu na wadau wengine wote tushirikiane kuhakikisha kwamba vyakula wanavyopata watoto wetu wanapokuwa mashuleni viwe salama kwa matumizi wasije wakajikuta wote wana mavitambi hivi,” amesema Dk Mtahabwa
Ameagiza vyakula hivyo vifanyiwe utafiti wa karibu na wadhibiti ubora wa kila halmashauri wafuatilie kuna nini kwenye shule zilizopo kwenye maeneo yao ili watoto walindwe kwa nguvu zote.
“Hatuna rasilimali inayoweza kulinganishwa na thamani ya watoto, hivyo ni lazima tushirikiane kuhakikisha chakula wanachopata shuleni ni salama,” amesema.
Ameongeza kuwa waraka wa mwaka 2023 umeweka msisitizo wa elimu ya kujitegemea kwa shule zote ili kuwajengea wanafunzi uelewa wa vitendo na kinadharia ili waweze kuzalisha chakula chao kwenye mazingira ya shule.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Swissaid Tanzania, Betty Malaki amesema mradi wa CRISP unaofadhiliwa na Kituo cha Utafiti cha Canada (IDRC), utatekelezwa kwa miaka mitatu kwa gharama ya Sh1.9 bilioni.
Amesema mradi huo utatekelezwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam, ukinufaisha jumla ya shule 48.
“Lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora na salama isiyo na madhara ya kiafya, huku tukiwapatia wakulima soko la uhakika kupitia kilimo hai,” amesema Malaki.
Naye, Ofisa Programu wa Sera kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Abiud Gamba amesema kimataifa shirika hilo linaunga mkono programu za lishe shuleni katika nchi 60, zikifikia mamilioni ya watoto kila mwaka.
“Ushahidi unaonyesha wazi kuwa milo ya shuleni huongeza uandikishaji na mahudhurio, huboresha umakini na ujifunzaji, na huleta faida kubwa kiuchumi,” amesema.Gamba
Amesema kuwa licha ya mafanikio yaliyopo nchini, bado kuna changamoto za upatikanaji wa lishe kamili shuleni, ikiwemo uhaba wa vyakula vya asili ya wanyama, mboga na matunda.
“Mradi wa CRISP unatarajiwa kusaidia kuimarisha uhusiano kati ya shule na jamii, kukuza kilimo ikolojia na kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora huku ukichochea maendeleo ya wakulima wadogo na uchumi wa ndani,” amesema Gamba.
