Mama lishe auawa usiku akitoka kazini, mwili watupwa shambani Moshi

Moshi. Simanzi imetawala katika Mtaa wa Mnazi, Kata ya Ng’ambo mkoani Kilimanjaro, baada ya mwanamke mmoja anayefanya biashara ya chakula, Restituta Moshiro (40), kukutwa ameuawa na mwili wake kutupwa kwenye shamba la mahindi, ukiwa na majeraha yanayoashiria aliburuzwa na kukabwa kabla ya kukutwa na mauti.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, Aprili 17, 2026, wakati mwanamke huyo, aliyekuwa akifanya biashara ya kuuza chakula kando ya barabara kuu ya Moshi–Arusha, eneo la Shaa Tours, akirejea nyumbani kwake.

Mwili wa Restituta, anayefahamika zaidi kama Mama Baraka, umekutwa ukiwa na damu puani, baada ya nguo yake ya ndani kukutwa imevuliwa na kutupwa pembeni ya mwili.

Pamoja na nguo hizo, vifaa alivyokuwa amebeba kwa ajili ya mwanaye wa miezi saba, ikiwemo maziwa, unga wa lishe na mwamvuli kwa ajili ya mvua, vilikutwa vimetapakaa hatua chache kutoka ulipo mwili wake.

Akizungumza katika eneo la tukio, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Moshi (OCD), Azizi Kalokola, amesema Jeshi la Polisi tayari limeanza upelelezi wa kina kubaini mazingira yaliyosababisha kifo hicho cha kutatanisha.

Eneo katika shamba ulipokutwa Mwili wa Restituta Moshiro (40) mkazi wa Mtaa wa Mnazi, Kata ya Ng’ambo. Picha na Yese Tunuka

“Mimi nina uhakika tukishirikiana na ninyi (wananchi) na sisi (Jeshi la Polisi) tutampata huyo aliyefanya kitendo hiki cha kumkaba na kumpeleka kwenye mahindi. Wamemkaba, maana anaonekana kama amekabwa mpaka ametoa damu,” amedai OCD Kalokola.

Kauli ya mama mwenye nyumba

Mama mwenye nyumba wa marehemu, Hilda Lyatuu, amesimulia tukio hilo, akieleza kuwa marehemu alikuwa mpangaji wake ambaye waliishi naye kwa maelewano makubwa na kusaidiana kulea mtoto wake mchanga.

Hilda amebainisha kuwa alikuwa na utaratibu wa kumpitia marehemu kazini kwake kila ifikapo saa 2:30 usiku kwa ajili ya kumchukua mtoto na kutangulia naye nyumbani ili kumpunguzia mzigo mama huyo wakati akiendelea na biashara zake.

“Jioni ilipofika, nikampitia, nikamwambia mimi naondoka. Akanambia sawa, lakini mtoto ameshatangulizwa na dada yake. Basi na mimi nikaondoka, nikamwacha pale saa mbili na nusu usiku,” amesema Hilda.

Ameongeza kuwa, usiku huo akiwa amelala, alishtushwa na sauti ya kilio cha mtoto mchanga wa marehemu aliyekuwa amelala na dada yake, jambo ambalo lilimfanya aamini kuwa mama huyo alikuwa ameshaingia ndani kwake, kama ilivyokuwa kawaida yao ya kusalimiana kila anaporejea.

“Nilisikia sauti ya mtoto analia usiku. Nikadhani labda ndiyo mama wa mtoto amerudi. Kumbe mama hajaingia. Asubuhi ndipo nikajua kupitia simu… nikaambiwa Mama Baraka amekutwa kwenye shamba amekufa,” amesimulia.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Moshi (OCD),Azizi Kalokola akizungumza na wananchi eneo lilipotokea tukio la mauji kata ya Ng’ambo. Picha na Yese Tunuka

Ndugu wa karibu wa marehemu, Lilian Kimario, ameelezea kuwa alikuwa mtu wa mwisho kuonana na Restituta kabla ya mauti kumfika, ambapo marehemu alifika dukani kwake kununua mahitaji ya mwanaye mchanga.

Lilian amesema kuwa marehemu alifika dukani hapo majira ya saa 2:30 usiku wa kuamkia leo na kuchukua unga kwa ajili ya kumlisha mwanaye, huku akionyesha kuwa na amani na bila dalili zozote za kuwa na mzozo na mtu yeyote.

“Sasa akaja akaniomba unga wa lishe wa mtoto. Nikamwekea pale dukani, akaondoka. Nikamuuliza, ‘Mtoto yuko wapi?’ Akanambia mtoto ameshatangulizwa na dada yake. Basi akaondoka kwa amani, wala hakukuwa na mzozo wowote, wala hatujawahi kugombana,” amesema Lilian.

Akisimulia jinsi alivyopata taarifa za kifo hicho, Lilian amesema: “Kipindi nafungua tu duka saa 1:30 asubuhi, kijana mmoja akaja… akaniambia, ‘Mama, umepata taarifa gani?’ Namwambia sijapata taarifa yoyote. Akasema, ‘Mama Baraka amekutwa kwenye mifereji.’ Yaani yule mama amefariki,” amesema ndugu huyo wa marehemu.

Diwani wa Kata ya Ng’ambo, Gadiel Mrema ametoa rai kwa wananchi kuwa walinzi wa wenzao, hususan katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo, akibainisha kuwa mashamba ya mahindi yaliyostawi yanaweza kutumiwa na wahalifu kama maficho ya kufanya matukio ya kikatili.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Moshi (OCD), Azizi Kalokola akizungumza na wananchi eneo lilipotokea tukio la mauji kata ya Ng’ambo. Picha na Yese Tunuka

Aidha, Mrema amehusisha mazingira ya tukio hilo na changamoto ya uuzaji wa pombe haramu ya gongo katika eneo hilo, akisisitiza kuwa ulevi unachangia kutokea kwa vifo vya kutatanisha na kutoa onyo kali kwa wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

“Kuna tatizo la uuzaji wa pombe haramu ya gongo hapa kwenye mtaa huu na karibu na eneo hili ambako limetokea tukio hili,” amedai.

Mwili wa marehemu Restituta, ambaye ameacha watoto wawili, akiwemo mmoja anayesoma chuo na mwingine mchanga wa miezi saba, umechukuliwa na Jeshi la Polisi na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo cha kifo chake.