LICHA ya Malindi kuwa katika hatari ya kushuka daraja msimu huu, uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi bado wana imani kubwa ya kubaki salama kwenye Ligi Kuu Zanzibar.
Meneja wa timu hiyo, Ramadhan Sanga amesema awali timu ilipoteza mwelekeo baada ya kuondokewa na mdhamini, lakini kwa sasa imeanza kurejea katika kiwango chake.
“Malindi haiwezi kushuka daraja. Bado kuna mechi nane mbele yetu na tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunabaki,” amesema Sanga.
Malindi ipo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi 22, tofauti ya alama moja tu na Polisi iliyo nafasi ya 13 na pointi 25.
Sanga alisisitiza tofauti hiyo ndogo ya pointi ndiyo inayowapa matumaini ya kubaki salama na wamejipanga kutumia nguvu na akili katika mechi zilizosalia.
Akizungumzia kipigo cha mabao 4-1 walichopata dhidi ya JKU Aprili 12, amesema kilitokana na baadhi ya wachezaji kuchelewa kujiunga na timu kabla ya mechi.
Amesema, mechi ijayo dhidi ya KMKM, wanajiandaa kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu ikiwa ni sehemu ya mkakati wao wa kutoshuka.
Meneja Sanga amewataka mashabiki wa timu hiyo wasife moyo na waendelee kuipa hamasa kwani imerudi na nguvu mpya ya kupambania malengo ya kutoshuka daraja.
