Dar es Salaam. Licha ya Serikali kwa nyakati tofauti kusisitiza mara kadhaa kuwa elimu ya msingi na sekondari katika shule za umma hutolewa bure, suala la michango shuleni limeendelea kuwa mjadala mzito katika jamii huku wazazi, walimu na wadau wa elimu wakieleza sababu mbalimbali zinazoifanya changamoto hiyo ionekane kuwa sawa na fupa gumu kwa wahusika.
Upungufu wa rasilimali katika baadhi ya shule, ongezeko la wanafunzi pamoja na mahitaji ya mara kwa mara ya uendeshaji wa taasisi hizo, vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea kuendelea kwa michango kwa wazazi, licha ya kuwepo kwa sera ya elimu bila ada iliyolenga kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi.
Aprili 9, 2026 mjadala huo uliibuka tena bungeni baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kueleza msimamo wa Serikali kuhusu michango hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Segerea, Agnesta Kaiza.
Mbunge huyo alitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali kukomesha michango holela inayotozwa katika baadhi ya shule, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wazazi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema Serikali haina tatizo na michango ya chakula shuleni pale inapokubaliwa na jamii husika kwa lengo la kuboresha lishe ya wanafunzi.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa michango mingine yote lazima ifuate mwongozo wa Serikali na ipate kibali cha mamlaka husika, hususan wakuu wa mikoa.
“Michango yote lazima ifuate utaratibu uliowekwa. Haiwezekani kila shule ikaibua tozo zake kiholela. Serikali imeweka utaratibu wa kugharamia huduma muhimu za elimu, hivyo shule hazipaswi kuwatoza wazazi michango isiyo rasmi,” alisema Dk Nchemba.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwananchi katika baadhi ya shule za umma unathibitisha kile kilichosemwa na mbunge huyo.
Katika Shule ya Sekondari Kipunguni iliyopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, mzazi mmoja alilieleza Mwananchi kuwa kila siku wamekuwa wakilipa Sh500 shuleni.
Anasema fedha hizo hugawanywa kwa utaratibu ufuatao: remedial (masomo ya marekebisho) (Sh300) mlinzi (Sh100) na walimu wa kujitolea (Sh100).
Mzazi mkazi wa Kinondoni, Mariam Abdallah amesema katika shule anayosoma mwanawe kuna michango kama ya madawati, ulinzi au matengenezo ya shule, ambayo wazazi hujulishwa kwa kutumiwa barua.
“Unaambiwa elimu ni bure, lakini mara unaletewa barua ya kuchangia madawati, mara ulinzi au matengenezo ya shule unajikuta ukipiga hesabu inafika hadi Sh80, 000 sasa unajiuliza hapa cha bure ni nini. Wazazi wengi tunachangia kwa sababu hatuna namna nyingine,” amesema.
Katika shule moja ya sekondari mkoani Arusha kuna mchango wa chakula, hosteli, wapishi, walinzi na afya unaofikia Sh300,000 kwa muhula, madarasa ya marekebisho (remedial) Sh25,000 kwa muhula, ujenzi wa uzio Sh50,000, dawati na kiti Sh100,000 na kitanda Sh200,000.
Suala la michango shuleni si geni katika mjadala wa kitaifa, mwaka 2018, Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alitoa agizo la kupiga marufuku michango ya kulazimishwa shuleni ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila vikwazo vya kifedha.
Akizungumza wakati huo, Magufuli alisisitiza hakuna mwanafunzi anayepaswa kurudishwa nyumbani kwa sababu ya michango.
“Ni marufuku watoto walioko shuleni kuchangishwa mchango wa aina yoyote. Nikisikia kuna shule ambayo watoto wanarudishwa nyumbani kwa sababu ya michango, mkurugenzi wa wilaya ajue hana kazi,” alisema.
Kauli hiyo ilikuja miaka miwili baada ya Serikali kuanza rasmi utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo mwaka 2016, ambayo ililenga kupunguza mzigo kwa wazazi na kuongeza fursa ya watoto wengi zaidi kujiunga na elimu ya msingi na sekondari.
Hata hivyo, Serikali imekuwa ikieleza kuwa pamoja na marufuku hiyo, bado wazazi wanaweza kushiriki katika maendeleo ya shule kupitia michango ya hiari inayokubaliwa na wazazi wenyewe kupitia kamati za shule.
Akizungumza katika moja ya mikutano ya hadhara, aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali haizuii kabisa wazazi kushiriki katika maendeleo ya shule, bali inapinga michango inayokusanywa bila utaratibu.
“Serikali haizuii kuchangia maendeleo ya shule. Kinachokatazwa ni michango ya ovyo ovyo isiyopitishwa na kamati za shule au wazazi,” alisema Majaliwa.
Kwa mujibu wa Serikali, michango inayoruhusiwa ni ile inayokubaliwa na wazazi kupitia vikao rasmi vya shule na haipaswi kuwa kigezo cha kumzuia mwanafunzi kuendelea na masomo.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pia imekuwa ikisisitiza kuwa ni kosa kwa shule kumfukuza au kumrudisha mwanafunzi nyumbani kwa sababu ya michango.
Aliyekuwa Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, aliwahi kueleza kuwa utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo unapaswa kuzingatiwa kikamilifu na viongozi wa shule.
“Ni marufuku kumfukuza mwanafunzi shule wakati wa utekelezaji wa waraka wa elimu bila malipo,” alisema Ndalichako, akisisitiza kuwa watoto wote wanapaswa kuendelea na masomo yao bila vikwazo.
Kauli hizo za mawaziri zinaungana katika eneo moja la wazazi kushiriki kuchangia elimu kwa makubaliano rasmi na michango iliyokubalika kwa utaratibu utakaowekwa, kama anavyofafanua Naibu Waziri wa Tamisemi Dk Festo Dugange.
“Wazazi wanatakiwa kushiriki kuchangia kwa makubaliano rasmi, kwa michango ambayo imekubalika kwenye kamati, bodi za shule, vikao rasmi vya wazazi na mkuu wa wilaya husika kujiridhisha kwamba mchango unaotakiwa si holela bali unasaidia kuboresha elimu. Tunaendelea kuwashauri wananchi kuwa na wajibu wa kushiriki wakati Serikali inaendelea kutoa ruzuku na elimu bila ada,” amesema.
Sawa na viongozi waliotangulia, Dugange amesema: “Pamoja na makubaliano hayo ya kamati, bodi ya shule na vikao cha wazazi hakuna mwanafunzi ambaye atakosa fursa ya kusoma kwa sababu mzazi wake hajachangia, kipaumbele chetu ni elimu ya mtoto.
Kuwaondoa wazazi wasishiriki kabisa katika elimu ya watoto wao tunaweza tukajenga utamaduni ambao mwisho wa siku utakuwa na changamoto, muhimu michango yote ni lazima iwe na sababu za msingi lakini iwe rasmi kupitia kamati, bodi, vikao vya wazazi na mkuu wa wilaya ajiridhishe,” amesema Dugange.
Suala hilo limesisitizwa na Waziri wa Elimu wa sasa, Profesa Adolf Mkenda kuwa elimu bila malipo haimaanishi wazazi hawapaswi kushiriki kabisa katika mahitaji ya watoto wao shuleni, lakini mchango huo haupaswi kuwa wa kulazimishwa.
“Ni muhimu jamii kushiriki katika maendeleo ya shule, lakini mtoto hapaswi kurudishwa nyumbani kwa sababu ya michango,” alisema Profesa Mkenda katika moja ya mikutano yake na wadau wa elimu.
Rita Manongi, mwalimu katika mojawapo ya shule za msingi jijini Dar es Salaam, amesema michango hiyo hutokana na mahitaji ya ziada ambayo wakati mwingine hayatoshelezwi kikamilifu na fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya uendeshaji wa shule.
Amesema kuna wakati shule hukabiliwa na changamoto kama matengenezo ya miundombinu, ulinzi wa shule na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia.
“Serikali inatoa fedha za uendeshaji wa shule, lakini wakati mwingine hazitoshelezi mahitaji yote. Ndipo kamati za shule huamua kushirikisha wazazi ili kutatua changamoto hizo,” amesema Manongi.
Mchambuzi wa masuala ya elimu Dk Elihuruma Massawe amesema mara nyingi changamoto hutokea pale ambapo shule zinakabiliwa na upungufu wa rasilimali, jambo linalowasukuma baadhi ya walimu au viongozi wa shule kutafuta michango kutoka kwa wazazi.
“Serikali ilifanya jambo kubwa kuanzisha elimu bila malipo, lakini changamoto ya rasilimali katika baadhi ya shule bado ipo. Hivyo wakati mwingine kunakuwa na jaribio la kukusanya michango ili kukidhi mahitaji ya shule,” amesema.
Baadhi ya wazazi waliozungumza na gazeti hili wamesema licha ya elimu kutangazwa kuwa bure, bado wanakutana na michango ya mara kwa mara kwa majina tofauti.
Juma Mwita mkazi wa Temeke Mikoroshini amesema wazazi wengi hulipa michango hiyo ili watoto wao wasipate changamoto shuleni.
“Ukikataa kuchangia, mtoto anaweza kuonekana kama hana ushirikiano. Hivyo wazazi wengi tunalipa ili watoto wetu wasipate usumbufu, unaambiwa unatakiwa kulipia masomo ya ziada Sh50, 000 kwa mwezi na ukiangalia unataka mtoto afaulu unakuwa huna jinsi zaidi ya kutekeleza,” amesema Mwita.
Kwa upande wake Neema Kessy, mzazi mwenye watoto wawili wa shule ya msingi amesema michango hiyo huwa changamoto kubwa kwa familia zenye kipato kidogo.
“Unapokuwa na watoto wawili au watatu wanaosoma, kila mchango mdogo unakuwa mzigo mkubwa kwa mzazi na wakati mwingine unalazimika kuumiza kichwa ili watoto wasipate shida huko shuleni,” amesema.
