Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikiana na Save the Children pamoja na Benki ya Stanbic Tanzania, imezindua mradi wa “Adopt an ECD Centre” unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma bora za Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) visiwani humo.
Uzinduzi huo uliofanyika jana Aprili 16, 2026 katika ofisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ulihusisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
Katika hatua ya kuunga mkono mpango huo, Benki ya Stanbic Tanzania imetangaza kutoa Sh500 milioni huku ikikabidhi kiasi cha Sh185 milioni kama sehemu ya awamu ya kwanza ya ufadhili.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZPDB, Profesa Mohammed Hafidh Khalfan amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya awali ya mtoto.
Amesema mchango wa wadau mbalimbali utasaidia kuendeleza programu bunifu na endelevu za ECD chini ya mpango wa kitaifa wa sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa amesema uwekezaji katika malezi ya awali ya mtoto ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Amebainisha kuwa mpango huo unaonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha kila mtoto anapata huduma bora, elimu ya awali na mazingira salama ya kukua.
Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Stanbic Tanzania, Derick Lugemala amesema benki hiyo inaendelea kuwekeza katika jamii kwa lengo la kuchochea maendeleo endelevu.
Amesema uwekezaji katika maendeleo ya awali ya mtoto ni muhimu katika kujenga msingi imara wa kujifunza na ustawi wa watoto.
Kwa upande wa Save the Children, mkurugenzi wake nchini Tanzania, Angela Kauleni amesema mpango huo utasaidia kuboresha huduma za malezi ya awali kwa watoto na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Mradi wa “Adopt an ECD Centre” unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi kwa watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi sita, ikiwemo elimu ya awali, afya, lishe na ulinzi wa mtoto.
Pia unalenga kuimarisha uwezo wa walezi na jamii katika kutoa malezi bora pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika maendeleo ya mtoto.
