Dkt. Mwigulu Awataka Watanzania Kudumisha Amani


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini akisisitiza kuwa mazingira ya amani ndiyo msingi muhimu unaowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wa taifa.

Amesema ni muhimu kwa wananchi kuwa makini na watu wanaohamasisha uvunjifu wa amani, akibainisha kuwa baadhi yao hufanya hivyo kwa maslahi binafsi. Alionya kuwa watu hao wasiruhusiwe kuihatarisha nchi, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani iliyopo.

Dkt. Nchemba ameeleza kuwa wanufaika wakuu wa amani ni wananchi wenyewe, hivyo wanapaswa kuilinda kwa nguvu zote ili kuendeleza shughuli zao za kila siku, ikiwa ni pamoja na biashara, kilimo na uwekezaji unaochangia maendeleo ya jamii.

Ameyasema hayo leo Ijumaa, Aprili 17, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kona ya Mbauda mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ambapo pia alikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara muhimu jijini humo.

Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara za Kilombero–Mbauda–Kisongo na Mbauda–Losinyai zenye urefu wa kilomita 13 ni sehemu ya maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, huku Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ili kurahisisha usafiri, kukuza biashara na kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na miradi hiyo.