Arusha. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amekemea tabia ya baadhi ya wakandarasi wanaolipwa fedha na Serikali kutekeleza miradi ya ujenzi nchini kushindwa kuwalipa watoa huduma walioingia nao mikataba kwa kisingia kuwa Serikali bado haijatoa fedha.
Ametoa kauli hiyo leo, April 17, 2026 wakati akipokea taarifa ya mradi wa ujenzi wa barabara za njia nne ya Mbauda hadi Losinyai, yenye urefu wa kilometa 27.5 na barabara ya Tanganyika Packers, Moshono Kona hadi Losinyai, yenye urefu wa kilometa 22.5 ambazo ni kati ya barabara zitawezesha miundombinu ya kufika ulipo uwanja mpya wa michezo wa Afcon.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha za malipo ya awali kwa wakandarasi kwenye miradi yote na hatafumbia macho makandarasi wasiowalipa wanaoingia nao mikataba ya utekelezaji wa huduma na vifaa kwa wakati na kuwasababishia usumbufu usio na sababu za msingi.
“Sitawavumilia wakandarasi wasiolipa fedha waliowapa kazi kwa wakati, tutawafuatilia, tukiwabaini tutawaweka kwenye kundi la kampuni ambazo hazifai kupewa za ujenzi hapa nchini,” amesema Dk Mwigulu.
Kuhusu ujenzi wa barabara hizo, amesema zitafungua jiji la Arusha kuwa wa kisasa, hivyo kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kufanya shughuli za kujipatia kipato na kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni utekelezaji wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan kuwapa huduma bora wananchi.
Amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, huduma za kijamii zimejengwa zikiwemo hospitali za wilaya 119 nchini, vituo vya afya zaidi ya 649, shule za amali zaidi 115 na upatikanaji wa huduma ya maji umeongezeka kupitia magari ya kuchimba visima virefu.
Katika hatua nyingine, amesema katika kutekeleza majukumu yake ya Waziri Mkuu, kwa mujibu wa Katiba, ana wajibu wa kushughulikia changamoto zozote na kwamba ataendelea kufanya hivyo bila kusita kwa sababu yapo kwenye mamlaka yake.
“Wapo wanaosema Waziri Mkuu anajishughulisha na mambo madogo madogo ya kusikiliza kero za kawaida za wananchi, nasema kila jambo linalomsumbua mwananchi lazima lipatiwe ufumbuzi kwa sababu Rais anataka kuwaachia wanachi tabasamu, tutapasua hadi mwamba kushughulikia changamoto za wananchi,” amesema Dk Mwigulu.
Awali, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali imetoa Sh17 bilioni, malipo ya awali kwa mkandarasi na Sh10 bilioni kimetolewa kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wanaopisha ujenzi wa njia nne kutoka Soko la Kilombero hadi Kisongo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano.
Amesema ujenzi wa barabara hizo utakua wa kisasa ukiwa pamoja na taa na mitaro mikubwa itakayoweza kuchukua maji ya mvua na kuwaondolea adha wananchi maji kuingia kwenye majumba yao pindi mvua kubwa zinaponyesha.
Mbunge wa Arusha Mjini ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda amesema licha ya miradi hiyo ya barabara ambayo inalenga kuboresha miundombinu ya jijini pamoja na kurahisisha mawasiliano wakati wa Afcon mwaka 2027, Serikali pia imetenga Sh400 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha mikutano.
“Huu ni wakati wa wana Arusha kuchangamkia fursa za kibiashara na kuacha siasa zisizo za maendeleo, Rais wetu ameweka mazingira mazuri kwa miradi ya soko la kisasa la Kilombero linajengwa, stendi ya kisasa na barabara hizi zikikamilika tupata mabasi ya mwendokasi kwenye jiji letu,” amesema Makonda.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Mhandisi Mohamed Besta amesema mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), imeanza ujenzi April 10, 2026, inatarajia kukamilisha April 9, 2027.