Watatu waliomuua ofisa mikopo Brac kwa kumnyonga ndani ya bajaji kunyongwa

Mbeya. Adhabu ya kifo sasa ni rasmi, baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kubariki adhabu ya kifo kwa wakazi watatu wa jijini Mbeya, waliomuua kwa makusudi, Ofisa mikopo wa Taasisi ya utoaji mikopo ya Brac, Victoria Manase.

Watu hao watatu, Alex Mwakimbwala, Elias Mushi au Mangi na Gidioni Ntulo au Mwankinga, walitekeleza mauaji hayo Juni 30, 2017 saa 5:25 asubuhi ndani ya bajaji, baada ya wauaji hao watatu nao kujifanya ni abiria.

Hukumu hiyo ya chombo cha juu cha rufaa za jinai hapa nchini, imetolewa Aprili 16, 2026 na majaji watatu, Rehema Mkuye, Sam Rumanyika na Ubena Agatho katika kikao cha mahakama hiyo kilichoketi jijini Mbeya.

Kulingana na ushahidi wa Jamhuri, Juni 30, 2017, Polisi jijini Mbeya waligundua mwili wa mwanamke ambaye ulitambuliwa kuwa ni wa Victoria Manase aliyekuwa Ofisa mikopo wa Brac, ukiwa umetelekezwa karibu na eneo la makaburi la Isyesye.

Awali ofisa huyo alitajwa kutoweka baada ya kukusanya Sh1.97 milioni za marejesho ya mikopo kutoka kwa wateja wa eneo la Isanga aliokuwa amewatembelea kwa ajili ya kutoa elimu ya mikopo na kukusanya marejesho.

Uchunguzi ulijikita kwenye simu yake ya kiganjani ambapo Polisi waliobobea katika uchunguzi wa uhalifu wa kiteknolojia, walichunguza mawasiliano yake ambayo yaliwaongoza hadi kwa watu waliokuwa wamenunua simu ya ofisa huyo.

Katika kamata kamata hiyo, kuanzia mtu wa kwanza aliyeinunua na baadaye kuiuza kwa mwingine, naye akaiuza kwa mtu wa tatu walikamatwa na ndipo wakamkamata mrufani namba moja, Mwakimbwala kuwa ndiye aliyeuza simu hiyo.

Mrufani huyo wa kwanza baada ya kukamatwa na kuhojiwa na Polisi, alikiri kushiriki mauaji hayo, na kuwataja washirika wenzake.

Ni ushahidi wa Jamhuri ulieleza kuwa siku ya tukio, Victoria (marehemu) alikuwa amepangiwa kutembelea maeneo ya Pambogo na Isanga ambapo alifanya vikao na wateja wenye mikopo Brac na kuondoka Isanga kurudi ofisini saa 5:25 asubuhi.

Wakati huohuo wakati Victoria anatoka eneo hilo la Isanga, kulikuwa na kundi la watu limepanga njama za kumuua wakishirikiana na mtu aliyetajwa ni Shaibu Mwinuka, aliyekuwa na wajibu wa kutoa ishara atakapomaliza tu kikao.

Baada ya Victoria kumaliza kikao, alikwenda kutafuta usafiri wa bajaji ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Lusekelo Atupele, ambapo mrufani namba moja hadi tatu yaani Mwakimbwala, Mushi na Ntulo, nao walipanda wakijifanya pia ni abiria.

Wakati bajaji ikiwa katika mwendo, Mushi alimnyonga Victoria kwa kusaidiana na washirika wenzake ambao ni Mwakimbwala na Ntulo hadi akakata roho.

Kufuatia Victoria kupoteza maisha, watatu hao walimpora fedha taslimu za marejesho ya mikopo pamoja na simu ya kiganjani aliyokuwa nayo kisha kuutelekeza mwili wake eneo la Isyesye kabla ya kugunduliwa na wananchi.

Shahidi namba moja wa Jamhuri, Leonard Magoma na Shahidi namba tisa, Zeinab Kesi ambao wote ni viongozi wa serikali ya mtaa, walitoa ushahidi wao wakielezea namna walivyoona mwili wa Victoria na kufuatilia njia waliyopita wauaji.

Kwa upande wake, shahidi namba tano, Sajini Daniel mwenye namba D.5517 alielezea namna alivyofanya ufuatiliaji wa mawasiliano ya simu ya marehemu kwa watu waliokuwa wameinunua ambao ni pamoja na shahidi namba sita na namba 14.

Baada ya kukamatwa kwa mashahidi hao na kuhojiwa, vidole vilimnyooshea Mwakimbwala kuwa ndiye aliyeuza ambao alikamatwa na kukamatwa kwake kukasaidia kupatikana kwa mrufani wa pili na tatu na wote walikiri kutenda kosa hilo.

Baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa pande mbili na maoni ya wazee washauri wa mahakama, Aprili 4, 2022 Jaji David Ngunyale wa Mahakama Kuu Mbeya, aliwatia hatiani watatu hao, na kuwaachia wawili akiwamo dereva bajaji.

Aliwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kuwa ndio adhabu pekee iliyotamkwa katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu au Penal Code.

Washitakiwa wakiwakilishwa na mawakili Felix Kapinga, Chapa Alfredy na Nyasige Kajanja walikata rufaa mahakama ya Rufani Tanzania, wakiegemea sababu nane.

Moja ya sababu ni kuwa hakuna shahidi wa Jamhuri aliyewaona au kuwakamata wakati wakimuua Victoria na kuwa kielelezo PE7 ambayo ni maelezo ya mrufani namba 1 na PE8 ya mrufani namba 3 yalichukuliwa wakati wawili hao wakiwa wameteswa katika kituo cha polisi na mmoja alikuwa na jeraha.

Walieleza kuwa hakuna maelezo yoyote ya onyo ya mrufani namba moja hadi 3 ambayo yalipokewa kama kielelezo PE13 ,PE9 na PE 11 ambayo yalichukuliwa mbele ya ndugu wa warufani wala wakili kama sheria inavyoelekeza.

Mbali na sababu hizo, walieleza kuwa ushahidi wa shahidi namba moja na tisa ulishindwa kuwaunganisha warufani na uhalifu huo kwa vile warufani hao walikuwa mikononi mwa polisi na walilazimishwa kwenda eneo ambalo mwili wa marehemu ulipatikana siku ya nyuma yake, kabla ya wao kukamatwa.

Halikadhalika walidai kuwa hakuna mrufani hata mmoja aliyekamatwa akiwa na simu ya marehemu ambayo ni kilelezo PE3 cha upande wa mashitaka, wakisema hiyo inamaanisha ile kanuni ya mtu kukutwa na mali ya wizi haikuthibitishwa.

Walisema utetezi wa warufani na vielelezo vyao vinaonyesha hawakuwepo eneo la tukio siku ya mauaji hayo, maelezo yao ya onyo na yale ya ungamo hayana muunganiko na mlinzi wa amani alithibitisha walikuwa na majeraha.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Alex Mwita akisaidiana na wakili wa Serikali, Veneranda Masai walipangua hoja hizo wakisema Jaji alikuwa sahihi alipotumia maelezo yao kuwatia hatiani.

Wakili Mwita alieleza kuwa wakati upande wa mashitaka ulipotaka kutoa maelezo hayo warufani walipinga na mahakama ikaenda kwenye kesi ndani ya kesi kuamua kama waliteswa au la na kuthibitisha waliyatoa wakiwa watu huru.

Kuhusu simu ya marehemu kuwa kulikuwa na mkanganyiko wa kama ni TECHNO Y4 au TECHNO W4, wakili huyo alisema shahidi wa watano wa Jamhuri alitumia namba maalumu ya utambuzi (IMEI namba), kufuatilia mawasiliano.

Katika hukumu yao, majaji hao walisema hakuna ubishi kuwa katika kuwatia hatiani warufani, Jaji aliyesikiliza kesi yao aliegemea katika maelezo ya ungamo  wa mrufani namba moja na namba tatu katika kesi hiyo.

“Ingawa maelezo hayo yalipingwa yasipokelewe kama kielelezo wakati wa usikilizwaji wa kesi kwa vile yalichukuliwa baada ya warufani kuteswa na polisi, Jaji aliyesikiliza aliyapokea baada ya kuridhika yalichukuliwa kwa hiyari.

“Mbali na hilo, Jaji aliona maelezo hayo yana ukweli kwa vile yaliungana na ripoti ya daktari ya sababu za kifo na mashuhuda wa mwili lakini namna maelezo hayo yalivyoeleza kwa kina hatua kwa hatua namna walivyofanya mauaji,” walisema.

Majaji hao walisema ingawa kulikuwa na utofauti wa jina la simu ya marehemu kama ni TECHNO Y4 au TECHNO W4,  simu hiyo ilipatikana kupitia namba zake za IMEI na hati ya ukamataji ilieleza tu kuwa ni aina ya TECHNO.

Walisema hiyo inaweza kuwa ilisababishwa na matamshi ya mashahidi katika utofauti wa Y4 na W4 kwa kuwa kuna mfanano lakini zaidi ni kuwa kutokana na uwezo wa mwanadamu, tukio hilo lilitokea 2017 nao wakatoa ushahidi 2022.

“Sisi hatukubaliani na hoja za mawakili wa warufani kuwa kulikuwa hakuna muunganiko (link) kati ya simu na mrufani wa kwanza. Kwa kuwa huo sio ushahidi pekee wa kuuegemea, tunaridhika kuwa kulikuwa na ushahidi mwingine mzito unaonyesha mrufani wa kwanza alishiriki katika mauaji hayo,” walieleza.

Hata hivyo, majaji hao walikubaliana na hoja ya mawakili wa warufani juu ya maelezo ya ungamo ya mrufani namba moja na tatu kuwa hayakuzingatia muongozo wa Jaji Mkuu katika kuyachukua, hivyo wanayaondoa katika rekodi za shauri hilo.

“Ikumbukwe kwamba kufutwa kwa maelezo hayo ya ungamo kwa mlinzi wa amani hakuzuii matokeo yetu ya awali, kwani ushahidi uliosalia wa maungamo ya mdomo na maelezo ya onyo ya warufani ni mzito,” walisisitiza majaji.

Kulingana na uchambuzi huo na wa ushahidi kwa ujumla wake, majaji hao walifikia hitimisho kuwa kesi ya upande wa mashitaka ilithibitishwa pasipo kuacha mashaka, hivyo rufaa hiyo haina mashiko na adhabu ya kifo waliyopewa ndio walistahili.