Nage, Mdako na Kukimbiza Kuku Kutikisa maadhimisho ya Muungano 2026

KATIBU wa michezo ya Jadi Wilaya ya Temeke, Juma Kilima, amesema chama hicho kipo tayari kwa ajili ya mapokezi ya timu zinazotokea visiwani Zanzibar kwa maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema, Chama hicho kimeandaa bonanza la michezo mbalimbali ya jadi, kati ya michezo hiyo, Nage na Mdako ndio itatoa bingwa.

Tumejiandaa na bonanza hilo na tutakuwa na ongezeko la timu kutoka Wilaya ya Ubungo, Kinondoni na Kigamboni,” amesema.

Katibu huyo amezitaja timu zilizopata nafasi ya kushiriki mashindano hayo kutokea Zanzibar ni Fighters Nage Queens ambayo ndiyo bingwa mtetezi, Chaani Queens na Mkoani Queens.

Amesema chama hicho kina jumla ya michezo 16 na katika bonanza hilo kutakuwa na mchezo wa mdako, kukimbia na Magunia, kukimbia na ndimu kwenye kijiko, kukimbiza kuku, kuvuta kamba na mingineyo.

Alieleza kuwa, mashindano hayo yatafanyika kwenye uwanja wa jadi wa Mbagala Zakhiem na wanatarajia bingwa kupata zawadi ya mchele, kombe na fedha.

Amesema, safari hii timu zinazotokea jijini Dar es Salaam hazitakuwa tayari kupoteza ubingwa huo.

Mbali na hilo, Katibu huyo amesema michezo hiyo ya jadi haipewi kipaumbele kwani inaonekana haitoi uwakilishi wa nje ya nchi.

Hivyo, endapo michezo hiyo itapewa kipaumbele itatoa uwakilishi mzuri tofauti na mingine ambayo imezoeleka duniani kote, huku akiwaomba wadau na mashirika kuwapa nguvu wanapohitaji msaada wa kuandaa mabonanza ya aina hiyo.