Dodoma. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kwa kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan wa maeneo ya vijijini kupitia usambazaji wa nishati ya umeme pamoja na nishati safi ya kupikia.
Ndejembi ametoa pongezi hizo leo, Aprili 20, 2026 Jijini Dodoma alipotembelea banda la Rea katika Maonyesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea ndani ya viwanja vya Bunge Jijini Dodoma
“Hongereni sana wataalamu mnatekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwafikishia wananchi wake kote nchini Nishati,” amesema.
Aidha, Ndejembi amewaalika wabunge kutembelea banda la maonyesho la nishati ili kushuhudia kazi inayotekelezwa na Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake.
“Tunawakaribisha waheshimiwa wabunge kutembelea maonyesho haya pamoja na wageni wao, kwani ni fursa nzuri ya kukutana na wataalamu na kujadili hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi katika majimbo yao,” amesema Ndejembi.
Amesema taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati zinashiriki na kwamba wataalamu wapo tayari na ni fursa kwa wabunge kukutana nao, ili kujadili changamoto zilizopo na kuangalia namna bora ya kuzipatia ufumbuzi.
“Lengo la maonesho haya ni kuonesha kazi iliyofanywa na Serikali, kuna mengi ya kujifunza kwenye banda hili,” amesema Ndejembi
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Rea, Hassan Saidy amemhakikishia Waziri Ndejembi kuwa, miradi yote inayotekelezwa kwa sasa itakamilika kwa wakati na Rea imejipanga kikamilifu kutekeleza miradi hiyo.
Rea ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika maonyesho hayo yaliyoanza leo.
