Mapya yaibuka fedha za vijana

Dar es Salaam. Licha ya Bunge kuidhinisha fedha za kutunisha mfuko wa maendeleo ya vijana kwa mwaka wa fedha 2025/26, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, imebaini Serikali haikutoa fedha hizo hadi kufikia Machi 2026.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, kitendo hicho kinakwamisha juhudi za kuwafikia vijana wengi wanaohitaji mikopo ya kuanzisha au kukuza shughuli za kiuchumi na hivyo kuathiri ustawi wao.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu Aprili 20, 2026 na mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Mchafu, wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Katika uchambuzi wake, kamati hiyo imeeleza wazi kutoridhishwa na hali hiyo, ikiitaka Serikali kutoa fedha hizo haraka ili mfuko huo ufanye kazi kama ilivyokusudiwa.

Hawa amesema kamati hiyo pia ilibaini mfuko huo uliendelea kutoa mikopo kwa kutumia salio la fedha kutoka mwaka uliopita, kiasi cha Sh336 milioni, kilitolewa kwa vijana katika mikoa ya Mwanza na Mtwara.

Aidha, amesema fedha nyingine zilikuwa katika hatua za mwisho kutolewa kwa vikundi vya vijana katika mikoa ya Mbeya, Arusha na Rukwa, jambo linaloonesha kuwa mahitaji ya mikopo bado ni makubwa.

Katika ziara yake mkoani Tanga, amesema kamati ilikagua utekelezaji wa mfuko huo kupitia kikundi cha vijana cha uzalishaji mali kilichofanikiwa kuongeza mtaji kutoka Sh100,000 hadi kufikia Sh52 milioni baada ya kupata mkopo wa Sh20 milioni.

“Mradi huo umezalisha ajira zaidi ya 20 na kutoa ujuzi kwa vijana zaidi ya 50, ukiwa mfano wa namna fedha hizo zinavyoweza kubadilisha maisha ya vijana endapo zitatolewa kwa wakati,” amesema.

Hata hivyo, amesema kamati imeonya kuwa mafanikio ya vikundi kama hivyo hayawezi kuwa ya kitaifa iwapo Serikali haitahakikisha upatikanaji wa fedha kwa wakati na kwa kiwango kilichoidhinishwa.