Tanga. Wakati shughuli ya kuwatafuta nahodha na baharia waliopotea kufuatia ajali ya meli ya MV Jozani 11 ikiendelea kwa siku ya tatu mfululizo bila mafanikio, manusura wa ajali hiyo, Abdul Mdogo ameeleza kwa kina namna tukio hilo lilivyotokea na mapambano yao ya kujiokoa baharini yalivyokuwa.
Akisimulia tukio hilo, Abdul Mdogo ni mmoja wa manusura wa ajali hiyo amesema walijinusuru kwa kujitosa majini katika juhudi za kuokoa maisha yao wakati hali ilipozidi kuwa mbaya ndani ya meli hiyo, iliyokuwa tayari imeanza kupoteza uthabiti wake.
Amesema haikuwa rahisi kutokana na mawimbi makubwa, upepo na baridi kali ya bahari iliyowakumba wakati wote walipokuwa wakielea majini.
Abdul ambaye ni baharia amesema, “Bandari ya Tanga tuliondoka saa moja na dakika arobaini na tano usiku na chanzo cha ajali ni mawimbi na upepo mkali kufuatia mvua kubwa iliyokuwa inanyesha,” anasimulia Abdul Mdogo akieleza mwanzo wa safari hiyo iliyogeuka kuwa mkasa mkubwa.
“Meli ilizama ghafla tulikuwa hatuna msaada wowote kwa kuwa maji yalikuwa yanatuvuta kati hatuendi kushoto wala kulia maji yanatuzungusha tu katikati,” amesimulia Abdul Mdogo kuhusu hali waliyojikuta nayo walipokuwa baharini.
“Hatukuweza kupata msaada kwa kuwa hakukuwa hata na jahazi wala meli iliyokuwa inapita wakati huo tulichokuwa tukifanya ni kumuomba Mungu tu,” amesimulia Abdul Mdogo.
Akieleza zaidi, amesema tukio hilo lilitokea kwa haraka sana kiasi kwamba halikutoa nafasi ya kufanya maamuzi ya kina au kuwasiliana na mamlaka kwa ajili ya kuomba msaada wa haraka.
Amefafanua kuwa hofu ilitanda miongoni mwa waliokuwemo ndani ya meli hiyo huku kila mmoja akijaribu kutafuta namna ya kuokoa maisha yake katika mazingira yaliyokuwa hatarishi na yasiyotabirika.
Wengine walifanikiwa kujitosa majini kwa wakati huku wengine wakishindwa kutokana na hali ya ghafla ya ajali hiyo.
“Kilichobaki ilikuwa ni kumuomba Mungu tu kwa sababu tuliona kabisa hatuna msaada wowote karibu nasi,” amesimulia Abdul Mdogo akieleza namna walivyokuwa wakitegemea imani yao katika wakati huo mgumu.
“Wakati mimi na wenzangu tulipoamua kujitosa majini, kapteni ambaye sasa hapatikani hakuweza kutoka kwenye meli na hatukujua ni nini kilitokea kwake.
“Kwa kuwa kila mtu alikuwa anaokoa maisha yake, haikuwa rahisi kujua kilichompata mwenzetu kwa wakati huo,” amesimulia Abdul Mdogo.
Amesema inawezekana hali ya meli ilipolala upande mmoja ilichangia baadhi ya watu kushindwa kutoka kwa wakati, jambo ambalo linaweza kuwa sababu ya kutopatikana kwa waliopotea hadi sasa.
Ameeleza waliobahatika kujiokoa walifanya hivyo kwa juhudi binafsi bila msaada wowote wa karibu.
“Huenda meli ilipolala upande wa kulia ilimchukua baada ya sisi kuruka na ndio maana hakufanikiwa kutoka,” amesimulia Abdul Mdogo akitoa mtazamo wake juu ya kilichoweza kutokea.
“Kwa ujumla tulikuwa 12 na wawili ndio hawajaonekana hadi sasa licha ya juhudi zinazoendelea,” amesimulia Abdul Mdogo.
Amesema walikaa majini kwa muda mrefu wakipambana na mawimbi makubwa pamoja na baridi kali iliyokuwa ikiathiri miili yao kadri muda ulivyokuwa unasonga mbele.
“Mungu ametusaidia tumepona tulipambana sana lakini si kwa nguvu zetu bali kwa rehema zake,” amesimulia Abdul Mdogo akieleza namna walivyookoka katika mazingira hayo magumu.
“Kila mtu alikuwa analia kivyake mwenzangu mmoja alikuwa analilia mkewe na watoto wawili akisema nani atawatunza,” amesimulia Abdul Mdogo.
“Alikuwa anaomba Mungu sana asipoteze maisha yake kwa ajili ya familia yake,” amesimulia Abdul Mdogo.
Amesema hali ya kisaikolojia ilikuwa ngumu sana kwa kila manusura aliyekuwa majini, ambapo baadhi walikata tamaa huku wengine wakijitahidi kuendelea kupambana hadi mwisho kwa matumaini madogo yaliyobaki.
“Mapema nilivyoona hali inazidi kuwa mbaya niliwapigia familia yangu kuwa meli imezama na kuwaambia kuwa si rahisi kupona katika hali hiyo tuliyokuwa nayo. Niliwaambia wakisikia taarifa wajue mimi ni miongoni mwa waliokuwemo na hiyo ilikuwa ni njia ya kuwaaga. Baada ya kukaa majini kwa saa nyingi tulipata msaada kutoka meli ya mafuta iliyokuwa inapita katika eneo hilo,” amesimulia Abdul Mdogo.
Waliokolewa na meli ya mafuta baada ya kuonekana wakielea majini wakiwa wamechoka sana na kupoteza nguvu kutokana na muda mrefu waliokaa baharini.
Hatua hiyo iliwapa nafasi mpya ya kuishi baada ya kupitia mateso makubwa yaliyotishia uhai wao kwa muda mrefu.
Amesema walipatiwa msaada wa awali kabla ya kufikishwa sehemu salama kwa ajili ya matibabu na mapumziko.
Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Tanga kuelekea Zanzibar ikiwa imebeba mzigo wa saruji pamoja na wafanyakazi, ambapo jumla ya watu 12 walikuwepo ndani ya chombo hicho kabla ya kukumbwa na ajali hiyo iliyosababisha kuzama ghafla baharini.
Watu 10 wameokolewa na kuthibitishwa kuwa salama huku wawili ambao ni nahodha na baharia wakiendelea kutafutwa katika Bahari ya Hindi.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), juhudi za uokoaji zinafanywa kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya usalama na wadau wa sekta ya usafiri wa majini, ambapo operesheni hiyo imekuwa ikiendeshwa mchana na usiku bila kusimama ili kuongeza uwezekano wa kuwapata waliopotea.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mamlaka ya Usafiri Bandarini Zanzibar ZMA, Suleiman Abdulla Salim amesema kuwa pamoja na changamoto za hali ya hewa, bado wanaendelea na msako huo kwa nguvu zote.
“Tunafanya kila jitihada kuhakikisha tunawapata waliopotea na hatutasitisha zoezi hili hadi pale tutakapopata majibu ya uhakika,” amesema Salim akieleza dhamira ya mamlaka hiyo katika operesheni hiyo.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali umeongeza nguvu kubwa katika shughuli hiyo na unaendelea kutoa matumaini kwa familia za waliopotea pamoja na jamii kwa ujumla.
Aidha, amebainisha kuwa meli hiyo ilikumbwa na mawimbi makubwa yaliyosababisha kupoteza mwelekeo kabla ya kuzama ghafla bila kutoa nafasi ya kutosha kwa waliokuwemo ndani kujiandaa au kuomba msaada.
Kwa upande wa mamlaka, zimeahidi kuendelea na hatua ya utafutaji hadi nahodha na baharia watakapopatikana huku zikiwataka wananchi kushirikiana katika kutoa taarifa zitakazoweza kusaidia operesheni hiyo.
Aidha, tahadhari imetolewa kwa watumiaji wa vyombo vya majini kuhakikisha wanazingatia usalama na kufuata miongozo ya hali ya hewa kabla ya kuanza safari.
