Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa wilaya za Kilosa na Mvomero, wameendelea kukumbwa na mafuriko, huku wengi wakilazimika kuishi katika kambi za muda.
Machi 2 mwaka huu, wilayani Mvomero zaidi ya kaya 700 zilikumbwa na mafuriko baada ya Mto Mbulumi kuvunja kingo kisha maji kuelekea katika makazi ya watu.
Hiyo si mara ya kwanza kwa mafuriko kuharibu mali na maisha ya watu mkoani Morogoro, kwa kuwa karibu misimu yote ya mvua changamoto hujitokeza, tofauti inaweza kuwa ni ukubwa, lakini maeneo kama Godegode na Mateteni Wilaya ya Mvomero yamekuwa yakikumbana na adha hiyo mara kwa mara.
Horo Mange, mkazi wa Mateteni ni miongoni mwa waathirika wanaosimulia machungu ya kupoteza kila kitu walichokuwa nacho kufuatia mafuriko yaliyotokea Desemba 28, 2025.
Akizungumza na Gazeti la Mwananchi jana Jumapili Aprili 19, 2026 Mange, mama wa watoto saba, anasema maisha yake yamebadilika ghafla baada ya maji kusomba mazao yake ya mpunga pamoja na kuharibu nyumba aliyokuwa akishi.
“Nilikuwa nalima mpunga, lakini wote umesombwa na maji. Nyumba niliyokuwa nikiishi nayo imeharibika kabisa, sasa hivi ninaishi kambini nikiwa na mtoto wangu wa wiki mbili,” anasema Mange kwa huzuni, akieleza kuwa, anatamani kurejea katika maisha yake ya awali.
Anasema hali ya maisha kambini ni ngumu kutokana na uhaba wa mahitaji muhimu na joto kali ndani ya mahema, hali inayowatesa zaidi watoto.
“Joto la kwenye tenti ni kali sana, hasa mchana watoto wanapata shida kulala,” anasema.
Fatuma Mupumuya ambaye ni Mwenyekiti wa Tenti Namba 1 katika eneo hilo, anasema pamoja na joto kali, changamoto nyingine kubwa ni maji kuingia ndani ya mahema wakati wa mvua.
“Hapa tupo wakazi 77, changamoto kubwa ni chakula. Lakini zaidi tunahitaji suluhu ya kudumu, kama kupewa maeneo mapya au kusaidiwa kuanza maisha upya, maana hatuna kitu chochote kilichobaki,” anasema Mupumuya.
Katika Wilaya ya Kilosa, hali si tofauti na iliyoko Mvomero, Khamis Pandu, mkazi wa Kata ya Kihonga anayeishi katika kambi ya Shule ya Msingi Kichangani Turiani, anasema walilazimika kukimbilia kambini baada ya kushindwa kumudu gharama za kupanga nyumba kufuatia uharibifu wa makazi yao.
“Vitu vyote vya ndani vimeharibika, maji yaliingia wakati niko shambani. Tulijikuta tumezingirwa na maji, tukalazimika kupanda juu ya miti kujiokoa,” anasema Pandu.
Pia, anasema kwa sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula na mahitaji mengine ya msingi, hali inayozidi kuwaweka katika mazingira hatarishi.
Kutokana na hali hiyo, Shirika la Misaada la Norwegian Church Aid (NCA), kwa kushirikiana na Anglican Church of Tanzania Diocese of Morogoro (ACDM), limeanza kutoa msaada wa kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko katika wilaya za Kilosa na Mvomero.
Msaada huo unalenga kuwafikia takribani watu 1,500 kati ya zaidi ya 3,000 walioathirika, ukiwalenga zaidi makundi yaliyo hatarini kama wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa NCA nchini, Theonat Mushi, lengo kuu ni kuhakikisha jamii zilizoathirika zinapata msaada wa haraka na wenye heshima.
“Kipaumbele chetu ni kuhakikisha jamii zilizoathirika zinapata msaada kwa wakati na kwa staha. Tunashirikiana kwa karibu na mamlaka za mitaa na viongozi wa jamii ili kuhakikisha misaada inawafikia wanaohitaji zaidi,” anasema Mushi.
Mratibu wa ugawaji wa misaada katika Jimbo la Anglikana Mvomero, Mathias Saanane anasema tayari kaya 160 zimefikiwa na msaada unaojumuisha magodoro, blanketi, ndoo zenye sabuni, taulo za kike pamoja na vifaa vya usafi.
Anaongeza katika kambi ya Turiani wamepeleka maturubai 40 yanayoweza kuhifadhi zaidi ya watu 200, pamoja na kugawa magodoro 51 kwa waathirika.
Diwani wa Kata ya Muhonda, Rashid Juma, amesema mafuriko yalianza Februari katika vitongoji vya Msufini na Madukani Kichangani, na hadi kufikia mwisho wa wiki iliyopita, nyumba 720 zilikuwa zimezingirwa na maji huku mali nyingi zikiwamo mifugo na chakula zikiathirika.
Anasema hadi sasa watu 70 wanaishi kambini, huku makazi yakizidi kuharibika siku hadi siku, akisisitiza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa chakula, hasa unga, huku akionya kuwa hali inaweza kuendelea kuwa mbaya zaidi.
“Hali ni mbaya, mito imehamia kwenye makazi ya watu. Inawezekana wakaendelea kuishi kambini kwa zaidi ya miezi miwili kwa sababu makazi yao yameharibiwa vibaya. Zaidi ya nyumba 1,830 zimeathirika katika kata hizi mbili,” anasema Juma.
Leo, bungeni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti Maalumu (CCM), Mkoa wa Morogoro, Sheila Lukuba alisema Serikali inachukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto ya mafuriko katika baadhi ya maeneo mkoani Morogoro.
Katika swali lake, Lukuba alieleza kata za Kihonda na Lukobe hazikuwa zikikumbwa na mafuriko hapo awali, lakini hali imebadilika kufuatia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ambao kwa kiasi kikubwa umechangia kuziba au kubadili mifumo ya asili ya mtiririko wa maji.
Alisema mafuriko hayo yamekuwa yakisababisha madhara makubwa kwa wananchi, ikiwamo kuharibika kwa mali na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akijibu swali hilo, Dk Dugange alisema Serikali imetambua uwepo wa tatizo hilo na imechukua hatua ya awali kwa kutuma timu ya wataalamu kufanya tathmini ya kina katika maeneo yaliyoathirika.
“Tumeshatuma wataalamu ambao wanafanya tathmini kubaini maeneo yanayohitaji miundombinu, aina ya miundombinu inayotakiwa pamoja na gharama husika. Baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kudhibiti na kuelekeza maji katika Mto Ngerengere,” alisema.
Alisisitiza kuwa lengo la hatua hiyo ni kupunguza athari za mafuriko na kurejesha hali ya usalama kwa wakazi wa maeneo hayo.
Katika swali la msingi, Lukuba ameuliza ni lini Serikali itajenga mfereji mkubwa wa kuelekeza maji katika Mto Ngerengere ili kunusuru wakazi wa kata za Kihonda na Lukobe ambao wamekuwa wakikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara nyakati za mvua.
Akijibu swali hilo, Dk Dugange alisema kata hizo zimeendelea kuathiriwa na mafuriko, na kwamba Serikali imepanga kujenga mfereji wa kuyaelekeza maji katika Mto Ngerengere kama suluhisho la kudumu.
Dugange alieleza kuwa tayari timu ya wataalamu imeundwa kufanya tathmini na kuandaa andiko la mradi litakaloainisha mahitaji halisi pamoja na mbinu sahihi ya utekelezaji.
Aliongeza kuwa kazi ya tathmini inatarajiwa kukamilika kabla au ifikapo Septemba 2026, hatua itakayofungua njia kwa utekelezaji wa mradi huo.
Serikali imewataka wananchi kuendelea kuwa na subira wakati taratibu za tathmini na upangaji wa bajeti zikiendelea, huku ikiahidi kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.
