Yona Amosi aifukuzia rekodi yake Ligi Kuu

KIPA wa Pamba Jiji, Yona Amosi amesema anapambania kuifikia rekodi ya msimu uliopita ambayo alimaliza akiwa na clean sheet 11, na anaamini hilo linawezekana katika mechi zilizosalia, hivyo anachokifanya ni kuzidisha bidii.

Amosi hadi sasa amefikisha clean sheet saba, ili zifike 11 zimebaki nne, jambo ambalo alisisitiza licha ya ugumu wa mechi na Ligi Kuu Bara kwa ujumla, anaamini katika kujituma hakuna linaloshindikana.

“Ingawa mechi ni ngumu bado nina nafasi na imani kubwa kuzifikia clean sheet 11 za msimu uliopita, sifanyi pekee yangu, ni kwa ushirikiano wa timu nzima pamoja na maelekezo ya benchi la ufundi kutupa mbinu kila wakati,” amesema Amosi na kuongeza;

“Pia nawafuatilia makipa wengine wanafanya kitu gani, mfano Patrick Munthali wa Mashujaa ni kipa mzuri sana, haijalishi msimu huu ana clean sheets chache, nachukua kinachonifaa kutoka kwake.”

Kwa upande wa Munthali ambaye msimu uliopita ndiye aliyeongoza kwa wazawa kwa kumaliza na clean sheets nyingi ambazo ni 12, hivi sasa ana tatu huku akisema anayeona atazifikia rekodi zake ni Amosi aliye na muendelezo mzuri.

“Amosi kajitahidi kuendeleza kile alichokifanya msimu uliopita, sina maana kwamba kipa mwenzangu Erick Johola hafanyi vitu vikubwa, ndiye anayeongoza kwa kuwa na cleansheets sita katika timu na msimu uliopita alikuwa na mbili, ila nazungumzia ambao msimu wa 2024-2025 tulimaliza na nyingi,” amesema.