Ugomvi wa baa wasababisha kifo Tabora, kijana achinjwa shingoni

Tabora. Ugomvi ulioanza kwa maneno makali ndani ya baa umegeuka kuwa tukio la mauaji baada ya kijana mmoja kudaiwa kuchinjwa na watu aliokuwa akinywa nao, tukio lililoacha simanzi kwa wakazi wa eneo la Usule mkoani Tabora.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, alisema tukio hilo lilimhusu Julius Mathew (27), fundi wa milango na madirisha, mkazi wa Usule, Kata ya Mbugani, Manispaa ya Tabora.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, marehemu alikuwa akinywa pombe katika baa moja akiwa na wenzake wanne, ambapo walizozana na kurushiana maneno makali kabla ya kuonekana kama wametulizana na kuondoka pamoja.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha walikorofishana wakiwa baa, baadaye wakaonekana wameelewana na kuondoka kwa kutumia pikipiki ya marehemu,” amesema Abwao.

Amefafanua kuwa baada ya kuondoka eneo hilo, kundi hilo lilipanda pikipiki ya marehemu iliyokuwa ikiendeshwa na mmoja wa watuhumiwa na kuelekea eneo la Usule, Miembe Mingi, ambako inadaiwa walimshambulia.

“Inadaiwa walimkata shingoni kwa kitu chenye ncha kali kisha kumtupa barabarani. Inaonekana walijifanya wameelewana ili kumshawishi aondoke nao kabla ya kutekeleza tukio hilo,” amesema.

Kamanda Abwao amesema watuhumiwa wote wanne wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi, huku baadhi ya vielelezo vikiwa tayari vimepatikana.

Miongoni mwa vielelezo hivyo ni pikipiki ya marehemu aina ya SANLG, ambayo watuhumiwa walikutwa wakijaribu kuisafisha damu iliyokuwa imeganda.

Amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini kwa kina chanzo cha tukio hilo na iwapo kulikuwa na sababu nyingine zaidi ya ugomvi wa baa ulioripotiwa.

“Tunasisitiza kuwa kutoa uhai wa mtu ni kosa la jinai na yeyote atakayebainika kuhusika atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria,” ameongeza.

Akizungumzia tukio hilo, mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete, Swaumu Kimaro, amehimiza wananchi kuepuka matumizi mabaya ya vilevi na dawa za kulevya vinavyoweza kuchochea maamuzi hatarishi.

“Matumizi ya kupita kiasi ya vilevi yanaweza kuathiri uwezo wa mtu kufanya maamuzi sahihi na wakati mwingine kusababisha vitendo vya ukatili kama hivi,” amesema Kimaro.