Mayanga arejea Mbeya City, kibarua hiki chamsubiri Ligi Kuu

Baada ya kuachana na Mecky Maxime, Mbeya City imemrejesha kikosini Salumu Mayanga kuwa kocha mkuu.

Mayanga anarejea baada ya kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita alipoiongoza wakati ikiwa Championship baada ya kupata ofa kutoka Mashujaa FC.

Kocha huyo anakuwa wa tatu kuifundisha Mbeya City msimu huu baada ya kutanguliwa na Malale Hamsin aliyepanda nayo Ligi Kuu, kisha Maxime aliyeachana nayo muda mfupi kupokea kipigo cha mabao 6-0 kutoka kwa Yanga.

Mayanga anajiunga na timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya akiwa huru kufuatia kuachana na Mashujaa FC na kibarua kizito ni kuinusuru kutoshuka daraja.

Kwa sasa Mbeya City imebakiza michezo 11 kuamua hatma ya kubaki au kushuka daraja, hivyo Mayanga itamfanya kutumia uwezo, uzoefu na mbinu zote kuendelea kulinda heshima yake katika medani za soka.

Kwa sasa Ligi Kuu imesimama kupisha michuano ya Kombe la Muungano, ambapo itarejea Aprili 30 ikiwa Mbeya City itakuwa nyumbani kukipiga dhidi ya Mashujaa kabla ya kuwavaa ndugu zao, Tanzania Prisons.