Dar es Salaam. Katika mfululizo wa makala zilizotangulia, Mwananchi imechambua kwa kina hali ya matumizi ya majengo yasiyokamilika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, yakitumika kwa biashara huku ujenzi ukiendelea juu na kuweka maisha ya wananchi hatarini.
Gazeti liliangazia jinsi majengo yanavyotumika kabla ya kukamilika na kukaguliwa, ajali na matukio ya moto yanavyoendelea kujirudia, pamoja na mgongano wa kanuni na udhaifu wa usimamimizi miongoni mwa taasisi mbalimbali zinazohusika.
Pia, limeangazia malalamiko ya viongozi wa mitaa kuhusu kukosa mamlaka na changamoto ya utekelezaji wa sheria zilizopo. Katika hitimisho hili, limeelekeza kwenye suluhisho la nini kifanyike ili kurejesha uwajibikaji, kuimarisha usimamizi na kulinda maisha ya wananchi.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi anasema kutokuwepo sheria iliyoandikwa moja kwa moja kuhusu kila hatua ya ujenzi, bado kuna mantiki ya kisheria inayowalazimisha wamiliki wa majengo kulinda usalama wa watumiaji na wananchi wanaopita karibu na majengo hayo.
Moja ya jengo linaloendelea kufanyiwa ukarabati Kariakoo.
Mwabukusi anasema kila hatua ya ujenzi, ina wajibu wa kisheria kabla ya kuanza ujenzi, hususani wa ghorofa, lazima yakaguliwe na kuthibitishwa, ndipo hutolewa vyeti (certificates) vinavyoruhusu ujenzi kuendelea.
“Ndiyo maana kuna vibali vya ujenzi na vyeti, hivi havitolewi kwa bahati mbaya, vinatolewa baada ya ukaguzi kuthibitisha usalama,” anasema.
Mwabukusi anasema kanuni za kisheria zinazojulikana kama Occupier’s Liability, ambazo zimetafsiriwa kutoka kwenye sheria za Uingereza na kukubalika kutumika katika mfumo wa sheria nchini.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, mmiliki au msimamizi wa eneo ana wajibu wa kuhakikisha eneo lake ni salama kwa mtu yeyote anayelitembelea au kupita karibu nalo.
“Ikiwa utanialika au utaniruhusu kutumia jengo lako, na nikapata madhara kwa sababu ya uzembe, una wajibu wa kisheria kunilipa fidia ya majeraha, maumivu na hasara niliyopata,” anasema.
Taasisi zisimamie wajibu wake
Anasema taasisi kama Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wahandisi wa majiji na mamlaka nyingine hutoa vibali baada ya ukaguzi wa usalama. Vibali hivyo vinapaswa kutolewa baada, siyo kabla ya ukaguzi kufanyika.
Moja ya jengo linaloendelea la ujenzi eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Mwabukusi anahoji kwanini maeneo yenye hatari wazi kama nguzo au mabomba yaliyoegemezwa vibaya na yanayoweza kuanguka huruhusiwa kuendelea kutumiwa na wananchi.
“Unaona kabisa kuna hatari, kuna vitu vinaweza kudondoka na kuua watu, lakini bado watu wanaruhusiwa kupita au kufanya biashara chini ya jengo. Kwa nini,” anauliza.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary anasema hali hiyo inaonesha haja ya Serikali kuanzisha mamlaka maalumu itakayoshughulikia masuala ya ujenzi pekee, yenye nguvu za kisheria kusimamia miradi yote ya ujenzi eneo la Kariakoo.
Omary anasema viongozi wa mitaa hawapaswi kubaki kama wasuluhishi wa migogoro midogo au wagongaji mihuri ya barua pekee, bali wapewe mamlaka ya kisheria kushiriki kikamilifu katika ukaguzi, kutoa taarifa za hatari na kusimamisha ujenzi unaokiuka taratibu kabla ya madhara hayajatokea.
Kamishna Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi anasema bila sheria na kanuni kusomana na kusimamiwa kwa pamoja, hatari zinazojitokeza Kariakoo zitaendelea kujirudia na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara na Taifa kwa jumla.
“Suluhisho si kutoa tu vibali vya biashara kuendelea, bali kuhakikisha sheria zote za ujenzi, usalama na matumizi ya majengo zinatekelezwa kikamilifu kabla ya jengo lolote kuanza kutumika,” anasema Mabusi.
Naye, Mwabukusi anasema si kila jambo lazima liwe na sheria ya moja kwa moja. Baadhi ya wajibu wa kisheria hutokana na mazingira na matendo, hasa pale usalama wa binadamu unapohusika.
Moja ya jengo linaloendelea la ujenzi eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Anasema changamoto kubwa ipo kwenye utekelezaji wa majukumu ya taasisi, kuanzia ngazi ya juu hadi ofisi za watendaji wa kata, ambako ndiko shughuli halisi za ulinzi na ukaguzi zinapaswa kufanyika.
“Hizi si kazi za kufanyika mara moja kwa mwezi au pale tatizo linapotokea, ni kazi za kila siku, ni mpango kazi,” anasema.
Pia, anasema umuhimu wa sasa ni kuziimarisha taasisi kuanzia ngazi ya kata kwa kuwapatia rasilimali watu na vifaa vya kutosha.
“Tunapoanzisha taasisi, lengo liwe kuzifikisha kwa wananchi, kazi halisi iko kwenye kata na mitaa, siyo ofisini tu juu, mamlaka inaanzisha taasisi na kusahau kuwa wanatumikia wananchi,” anasema.
Anasema taasisi tote zinazohusika kwenye ujenzi wawekwe watu kwenye ofisi za kata na Serikali za mtaa; na kuwapa kibali cha uamuzi ikiwamo ukaguzi wa majengo na utoaji wa vibali vya matumizi na sio wao kupewa kazi za kutoa barua kwa wananchi.
Kwenye masuala ya usalama, Maziku anasema changamoto kubwa iliyopo ni kutokuwepo kwa uratibu wa kisheria unaozifanya taasisi mbalimbali zinazohusika na ujenzi kufanya kazi kwa mfumo mmoja.
Anasema kama Sheria ya Mipango Miji, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) na kanuni za zimamoto mara nyingi hufanya kazi kwa kujitegemea bila mfumo wa pamoja wa utekelezaji.
“Sheria zetu zisipoongea lugha moja, ajali zitaendelea na lawama zitabaki kurushwa kutoka taasisi moja kwenda nyingine,” anasema.
Anasema mfumo wa utoaji vibali vya muda wa matumizi ya majengo umejaa mianya ya kisheria, kwani vibali hutolewa bila ushirikishwaji wa lazima wa wadau wote muhimu, akitaja Osha, Jeshi la Zimamoto na wachora ramani.
Mtaalamu wa masuala ya ujenzi, Diana Mkongole anasema matumizi ya majengo ambayo hayajakamilika eneo hilo, yanahitaji ushirikianao wa watu wengi.
Anasema hatua ya kwanza ni Serikali za mitaa na halmashauri kufanya ukaguzi wa kina wa majengo yote ambayo hayajakamilika lakini yanaendelea kutumika kwa biashara, maghala au makazi.
“Wafanye ukaguzi wa kina kwa yale ambayo yameanza kutumika, yawe ni mwisho, mengine yaendelee kujengwa na watu waombe vibali kulingana na uwezo wa fedha zao ili kumaliza ujenzi,”anasema Diana.
Mhandisi wa Jiji, Isack Mtega anasema jiji limeanzisha Partial Certificate of Occupation inayoruhusu matumizi ya sehemu ya jengo kwa masharti maalumu ya kiusalama, ikiwamo ujenzi kufanyika usiku, mwisho wa wiki au sikukuu ili kuepuka kuhatarisha wafanyabiashara na wanunuzi.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa endapo masharti hayo yatakiukwa, kibali hufutwa na ujenzi husitishwa mara moja.
Aidha, anasema tayari wamewasilisha mapendekezo ya kuwepo kwa sheria maalumu itakayodhibiti majengo pekee ili kuondoa muingiliano wa majukumu kati ya taasisi za Serikali.
