Jina la kujipachika halifuti jina halisi. Vijana wengi hasa wasanii hutembea na majina kama mzuka wa kubadili hali ya hewa. Utaona wakijipa majina makubwa kama Afande, Kanali, Meja, Killer, Simba, Dudu na mengine yanayofanana na hayo. Ni lazima watohoe majina ili kujiongeza. Mwite mtoto Kidawa, akiingia kwenye sanaa atajiita ‘Baby Kiddy.’
Hii ni hali ya vijana wetu kujipandisha mzuka ilimradi awe wa kipekee. Kwa heshima ya babu yake unamwita mtoto Dikusele, yeye analigeuza Dickson. Akipata hela atajiita Don Dick kulingana na hadhi yake ya wakati huo.
Hata hivyo majina hayo yatapita na nyakati, lakini majina yao ya asili ndiyo yatakayobaki salama. Nina maana uhalisia hudumu, ndiyo maana tunasema “mwongo hana kumbukumbu”.
Zamani tulidanganywa kuwa asili ya mwanadamu ni nyani. Lakini karne nyingi zikapita bila nyani kugeuka binadamu. Hatukatai kwamba kuna watu waliofanana na nyani, lakini hicho sio kigezo kwamba walitokana nao. Mbona hatuambiwi asili ya mamba ni kenge? Hata kama kungekuwa na mabadiliko endelevu, huyu binadamu angeendelea kubadilika na kuwa tai.
Maisha yana uhalisia wake. Mabadiliko hayakosekani, lakini asili ya maisha hubaki palepale. Tajiri alizaliwa mtupu kama masikini, alipumua, akala, akaenda haja, akazeeka na hatimaye akafa. Hakuna tajiri aliyewahi kuepuka kifo kwa kutumia pesa zake.
Japokuwa wapo watu wanaojisahau baada ya kuishi kama walio peponi, lakini hukumbushwa kuwa wao ni sawa na wengine kwa kuugua na hata kufa.
Wanadamu wote wana mahitaji yao ya msingi yanayofanana. Awe masikini au tajiri, mzungu au Mwafrika, mwanaume au mwanamke – wote mahitaji yao yanafanana.
Ndio maana wakimkuta mwenzao ameanguka njiani, watamsaidia hata kama hawezi kujieleza. Hii inathibitisha kuwa wanajua kuna alichokikosa, hivyo watajaribu kumpatia huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka kwenye uchunguzi maalum.
Kwa ufupi kila Mtanzania anahitaji maisha mazuri. Maisha haya ni ya uhakika wa chakula bora, mavazi bora na malazi bora. Tunafanya kazi na biashara, hivyo tunahitaji pia usafiri wetu na bidhaa zetu kwa uhakika. Mitikisiko ya uchumi isitufanyie utofauti kati ya masikini na matajiri. Matabaka haya mawili yanaonekana wazi kuwepo, lakini Serikali haina budi kupunguza utofauti wake.
Katika wakati huu mgumu wa vita ya Iran dhidi ya Marekani na swahiba wake Israel, upatikanaji wa mafuta umekuwa kitedawili. Bei ya mafuta imepanda na kuathiri upatikanaji wa mahitaji ya msingi kwetu sote.
Tunategemea tuwe wamoja katika kutafuta namna ya kupambana na hali hii. Sasa tunaposikia baadhi ya wabunge wetu wakihimiza ongezeko la tozo kwa wananchi, tunadhani wao hawaumizwi na ugumu huo.
Wengine wanawaza kuwa kuongeza tozo kutasaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya mafuta kwa wananchi. Lakini ukweli ni kwamba kabla ya kuongeza, tayari wananchi wanaumizwa na bei hizo. Kwa mfano uchumi wa mzazi anayesafirisha wanawe kwenda shuleni. Kwa mshahara wa kawaila hilo ni jambo gumu sana. kama waheshimiwa wabunge wakivaa viatu vya mzazi huyu, bila shaka wataelewa.
Zamani tulisikia simulizi ya kuku aliyeishi msituni kama wanyama wengine. Baridi kali ikatanda na kuhatarisha maisha ya wanyama. Kwa kuwa walishamwona binadamu akijihami dhidi ya baridi kwa kuota moto, nao kwa ujumla wao waliamua kumtuma kuku aende kuomba moto kwa binadamu. Kuku alipofika kwa binadamu alikuta anasa nyingi hata akaamua kuishi huko.
Hii ndiyo taswira ya wabunge wetu, watoto wa wakulima na wafanyakazi. Tumewatuma wakatuwakilishe kwa Serikali, lakini wanapopata unafuu wao wanasahau machungu yetu.
Wanakuwa kama kuku aliyeamua kuwaacha waliomtuma na kuzamia nyumbani kwa mwanadamu. Wanaitaka Serikali kutumia vyanzo vilevile kuongeza mapato badala ya kubuni mbinu mpya za kumkwamua mwananchi. Je, wamekosa ubunifu?
Masikini anatwikwa mzigo mkubwa zaidi wa gharama. Kwa kuwa anatumia kipato chake kujikidhi kwa kodi ya pango, usafiri, mavazi na chakula, bei ya mafuta ikipanda na nauli yake itapanda.
Bei ya chakula na bidhaa itapanda wakati kipato chake kinabaki kama kilivyo. Maisha yake yatakuwa magumu zaidi pengine kuathiri utendaji wake wa kazi, mahudhurio ya wanawe shuleni na afya zao kwa ujumla.
Haya yote yana athari kubwa kwa ukuaji wa uchumi. Mwananchi wa kawaida hulazimika kutumia usafiri wa umma, bodaboda, bajaji na taxi mtandao.
Hivyo havikwepeki kwani kuna wanaoishi kando ya mji, wapo wanaosafirisha bidhaa kila siku na wale wanaosafiri mikoani kwa kazi zao.
Gharama kubwa za usafiri huongeza gharama za uzalishaji viwandani na mashambani. Jambo hili linaweza kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa zima.
Kutokana na athari hizo, kumekuwa na wito kwa serikali kupunguza au kufuta tozo hizo. Wabunge wasichoke kuelezea uhalisia wa maisha yetu ya mtaani, lakini pia kukusanya maoni yetu juu ya urekebishwaji wa hali ya maisha.
Kama vile Mkuu wa Mkoa alivyotaka maoni ya wananchi namna ya kupunguza foleni za barabarani, nao wafanye hivyo kuepuka tozo na kubuni vyanzo vipya vya mapato. Tunaona wenzetu wakiwemo Kenya wanafuta baadhi ya tozo. Wao wamewezaje?
