Barker aruka viunzi vitatu Simba

KUINGIA kwa Steve Barker ndani ya Simba kulikuja katika kipindi kigumu ambacho kilihitaji zaidi ya mabadiliko ya kawaida ya benchi la ufundi, ilikuwa ni hatua ya kuanza upya kwa timu iliyokuwa inapoteza mwelekeo huku presha kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka ikiongezeka.

Kocha huyo kutoka Afrika Kusini, aliwasili Desemba 2025, wakati msimu ukiendelea ambapo mara nyingi timu huwa tayari zimeshajipanga kimfumo na kiuchezaji. Hali hiyo ilimuweka kwenye nafasi ya kufanya uamuzi wa haraka huku akitakiwa kupata matokeo ya papo hapo.

Katika mazingira hayo, Barker akizungumza na Mwanaspoti, alikiri wazi kuwa kazi ya kurejesha heshima ya Simba haikuwa nyepesi. Kauli hiyo ilionesha ukubwa wa changamoto alizokutana nazo tangu siku ya kwanza.

Moja ya changamoto kubwa ilikuwa ni ushindani wa ligi, hasa dhidi ya wapinzani wao wakuu Yanga na Azam. Ndani ya hali hiyo, Barker alilazimika kujenga timu mpya huku mashindano yakiendelea hali ambayo si rahisi kwa kocha yeyote.

Dirisha dogo la usajili mara nyingi hutumika kwa maboresho machache lakini kwa Simba hali ilikuwa tofauti kabisa. Klabu ilifanya usajili mkubwa uliobadilisha sura ya kikosi kwa kiwango kikubwa.

Majina makubwa yaliingia, akiwemo Clatous Chama, aliyerejea kuongeza ubunifu katika eneo la kiungo mshambuliaji.

Sambamba na hilo, Libasse Gueye mwenye mabao manne kwenye ligi na Anicet Oura mwenye mabao matatu wameongeza nguvu mpya katika safu ya ushambuliaji, wakiongeza kasi na ubunifu katika maeneo ya pembeni.

Katika safu ya ulinzi, waliingia Ismael Olivier Toure ambaye ni beki wa kati, ameongeza utulivu na uzoefu mkubwa, jambo lililoimarisha ngome ya timu hiyo huku akicheza sambamba na Rushine De Reuck aliyekuwa hapo tangu mwanzo wa msimu.

Katika beki ya kushoto, Nickson Kibabage amejidhihirisha kama mbadala wa Mohammed Hussein aliyeondoka huku Djibrilla Kassali akitulia golini akichukua nafasi ya Moussa Camara ambaye ni majeruhi wa muda mrefu.

Mabadiliko hayo ya ghafla yalikuwa mtihani mkubwa, kwani kuunganisha wachezaji wengi wapya kwa wakati mmoja kunahitaji muda na maandalizi ya kutosha.

Hata hivyo, Barker ameonyesha uwezo wa kuleta muunganiko wa haraka, jambo lililoanza kuzaa matunda uwanjani.

MBINU NA UTAMBULISHO MPYA WA UCHEZAJI

Mbali na mabadiliko ya kikosi, Barker ameanza kuipa Simba sura mpya ya kiuchezaji. Timu imeanza kuonyesha nidhamu katika kujilianda ikiwa ni timu ya tatu iliyoruhusu mabao machache zaidi katika ligi (7) huku ikiwa na mpangilio mzuri katika kushambulia.

Eneo la kiungo imekuwa sehemu muhimu, kuhakikisha mpira unasogezwa kwa haraka kutoka nyuma kwenda mbele, kazi hiyo imekuwa ikifanywa na Yusuph Kagoma, Alassane Kante pamoja na viungo wengine washambuliaji akiwemo Chama.

Wachezaji wa pembeni, Oura, Guaye, Elie Mpanzu wakitumika zaidi kuongeza kasi ya mashambulizi huku washambuliaji wa kati wakipata nafasi nyingi za kufunga.

Mfumo huu umeifanya Simba isiwe tegemezi kwa mchezaji mmoja, bali kucheza kama timu yenye muunganiko wa pamoja.

Ni mabadiliko yanayoonekana taratibu, lakini yenye msingi imara wa mafanikio ya muda mrefu. Japo changamoto inayoonekana kuwepo katika muundo wao wa uchezaji katika mfumo wa 4-2-3-1 ua 4-3-3 ni eneo la mwisho la ushambuliaji ambalo limekuwa likimtegemea zaidi Seleman Mwalimu ‘Gomez’ mwenye mabao sita ambaye hata hivyo ameshindwa kuwa na uwiano mzuri wa utumiaji nafasi.

Changamoto nyingine kubwa aliyokutana nayo Barker ni presha ya matokeo. Simba ni klabu yenye matarajio makubwa, ambapo ushindi si chaguo bali ni lazima.

Kocha huyo alirithi kikosi kutoka kwa Dimitar Pantev katika kipindi ambacho mashabiki walihitaji mafanikio ya haraka.

Kupoteza mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya Azam kuliongeza presha, hali iliyohitaji utulivu kutoka kwa benchi la ufundi.

Licha ya hilo, Barker ameweza kuhimili presha hiyo na kuendelea kujenga timu yake taratibu.

Hadi sasa, Simba imekusanya pointi 42 katika mechi 19 za ligi, ikiwa katika nafasi ya pili.

Tofauti ya pointi tano dhidi ya vinara wa ligi inaonyesha kuwa bado ipo kwenye mbio za ubingwa.

Haya ni matokeo yanayoashiria kazi kubwa inayofanywa nyuma ya pazia.

Akizungumzia hayo yote, Barker alisema: “Nilichokifanya kwanza ni ilikuwa ni kujenga msingi wa timu ikiwa ni pamoja na nidhamu, umoja na uelewa wa mbinu.

“Haikuwa rahisi kuunganisha wachezaji wengi wapya bila maandalizi ya muda mrefu lakini kwa kufanya kazi kwa karibu na wachezaji, tumepata muunganiko na naamini kuna mengi mazuri yanakuja.

“Ninaamini katika kujenga timu yenye usawa ulinzi imara na mashambulizi yenye ufanisi. Hii ni safari, hatujafika tunapotaka kufika bado.

“Lakini kila siku tunaendelea kuboresha na lengo letu ni moja kuirudisha Simba kwenye kiwango chake cha juu na kuwapa mashabiki furaha wanayostahili.