Morogoro. Siku chache kabla ya maporomoko ya tope kutokea katika kitongoji cha Waga, Kijiji cha Dimilo wilayani Morogoro, wakazi walianza kushuhudia dalili zisizo za kawaida ardhi ikipasuka na kutitia baada ya mvua kubwa, lakini hawakutambua hatari iliyokuwa inakuja.
Wakizungumza na Mwananchi, wananchi hao wamesema mvua kubwa zilizonyesha kabla ya tukio hilo ziliacha alama za nyufa katika eneo lililokuja kuwa chanzo cha maporomoko, hali iliyopuuzwa kutokana na kukosekana kwa tahadhari au taarifa rasmi kutoka kwa wataalamu.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Leonard Mkude amesema licha ya kuona mabadiliko hayo ya ardhi, hawakutarajia janga la kiwango hicho, lililoanza Aprili 16, 2026 na kuendelea hadi sasa, likisababisha uharibifu mkubwa wa mali na mazingira.
Amesema kaya 20 zenye jumla ya watu 62 zimelazimika kukimbia makazi yao kutokana na hatari inayoendelea, huku zaidi ya hekari 80 za mazao ya chakula na biashara ikiwemo karafuu, hiriki, mdalasini, pilipili, mtama, mihogo na migomba zikifunikwa au kusombwa na tope.
“Hali ni mbaya, watu wamepoteza makazi na mashamba yao. Wengi wanahifadhiwa kwa ndugu kwa sababu hatuna miundombinu ya kuwahifadhi sehemu moja. Tunahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu,” amesema Mkude.
Maporomoko ya tope kutoka Mlimba Mongwe yakiwa yamesambaa kwenye eneo la shule ya msingi Dimilo iliyopo kata ya Kibungo juu tarafa ya Matombo wilaya ya Morogoro. Picha Hamida Shariff
Ameongeza kuwa tukio kama hilo liliwahi kutokea miaka ya 1976 hadi 1977, lakini halikudumu wala kusababisha hasara kubwa kama ilivyo sasa, jambo linaloibua hofu na maswali kwa wananchi kuhusu chanzo cha tukio hilo.
Mmoja wa waathirika, Bertine Kung’alo, amesema amepoteza kila kitu nyumba na mazao na kwa sasa anaishi kwa ndugu huku akikosa mwelekeo wa maisha yake ya baadaye.
“Nilitegemea mashamba yangu kwa maisha, sasa sina chochote. Naiomba Serikali na wasamaria wema watuone, hali ni ngumu sana,” amesema.
Kwa upande wake, dDiwani wa Kata ya Kibungo Juu, Emiry Msimbe amesema hali ya wananchi si ya kuridhisha, akiiomba Serikali kufanya tathmini ya haraka na kutoa msaada kwa waathirika.
Amesema tayari shule ya msingi Dimilo imefungwa kufuatia kuzingirwa na tope, huku maandalizi yakiendelea kuwahamishia wanafunzi katika shule jirani ili waendelee na masomo.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema wataalamu kutoka taasisi mbalimbali wakiongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) tayari wameanza utafiti kubaini chanzo cha maporomoko hayo.
Maporomoko ya tope kutoka Mlimba Mongwe yakiwa yamesambaa kwenye eneo la shule ya msingi Dimilo iliyopo kata ya Kibungo juu tarafa ya Matombo wilaya ya Morogoro. Picha Hamida Shariff
“Hata hivyo, changamoto bado ipo kwani tope linaendelea kuporomoka, hivyo wananchi wanapaswa kuwa na tahadhari na subira wakati Serikali ikiendelea kushughulikia hali hii,” amesema Kilakala.
Maporomoko hayo yalitokea ghafla majira ya mchana Aprili 16, yakitanguliwa na kishindo kikubwa na muungurumo, hali iliyosababisha taharuki kubwa na uharibifu wa ardhi katika eneo hilo.
