Wabanguaji wa korosho watoa kilio chao

Mtwara: Licha ya jitihada za Serikali ya Tanzania kuweka mikakati ya kukuza sekta ya ubanguaji wa korosho na kufikia lengo la kubangua zaidi ya tani 600,000, sawa na asilimia 60 ya uzalishaji ifikapo mwaka 2030, bado sekta hiyo inaendelea kukabiliwa na changamoto zinazokwamisha matarajio hayo.

Kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Korosho Tanzania, nchi huzalisha wastani wa tani 300,000 hadi 500,000 za korosho ghafi kwa mwaka, lakini chini ya asilimia 20 ndizo huchakatwa ndani ya nchi, huku zaidi ya asilimia 80 zikiuzwa katika mataifa ya Vietnam na India kama malighafi.

Katika juhudi za kubadili hali hiyo, Chama cha Wabanguaji wa Korosho Tanzania (TACP) kimeiomba Serikali kuongeza juhudi katika kuwawezesha wabanguaji kwa kushughulikia vikwazo vinavyowakabili ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza thamani ya zao la korosho nchini.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika leo, Aprili 22, 2026, Fakhii Mussa, mbanguaji kutoka Mtawanya Juu, Manispaa ya Mtwara Mikindani, amesema kasi ya ukuaji wa sekta ya ubanguaji itaongezeka iwapo wabanguaji wadogo watawezeshwa kwa vitendo.

Amesema miongoni mwa changamoto kubwa ni ukosefu wa teknolojia za kisasa na vifaa vya ubanguaji, hali inayopunguza uzalishaji na ushindani wao sokoni.

“Iwapo tutapata nyenzo za kisasa na mafunzo ya teknolojia, naamini tutaleta mabadiliko makubwa katika sekta hii na kusaidia kufikia malengo ya Serikali,” amesema Fakhii.

Baadhi ya wabanguaji wa korosho wakiwa kwenye mkutano mkuu wa nne mkoani Mtwara.

Inaelezwa kuwa sekta ya ubanguaji ina uwezo wa kuajiri zaidi ya watu 100,000, wengi wao wakiwa wanawake na vijana, endapo uwekezaji na mazingira rafiki vitaimarishwa.

Wajumbe hao wamesisitiza kuwa hali hiyo ikiachwa iendelee, itaathiri kasi ya ukuaji wa sekta hiyo na kupunguza fursa za ajira, hususan kwa vijana na wanawake ambao ndio nguvu kazi kubwa katika shughuli za ubanguaji.

Akichangia hoja hiyo, Lidya Jacob kutoka Kisarawe, mkoani Pwani, amesema ucheleweshaji wa vibali vya kusafirisha malighafi unakwamisha shughuli za wabanguaji na kusababisha hasara.

“Tunapopata vibali kwa wakati tunafanya kazi kwa ufanisi, lakini mifumo iliyopo ni migumu na inachukua muda mrefu kupata majibu,” amesema Lidya, akiongeza kuwa hata leseni za ununuzi wa korosho katika soko la awali hupatikana kwa kuchelewa.

Akizungumzia kwa mtazamo mpana wa sekta, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wabanguaji wa Korosho nchini (TACP), Daniel Marwa, amesema sekta binafsi ndiyo mhimili mkuu wa ubanguaji, hivyo ushirikiano wake na Serikali ni muhimu katika kuongeza tija na ushindani.

Amesema moja ya maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele ni usimamizi mzuri wa soko la awali ili kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa malighafi.

“Ukuaji wa sekta ya ubanguaji nchini kwa kipindi cha hivi karibuni umechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa soko la awali, hivyo ni muhimu kuendelea kuliboresha,” amesema Marwa.

Ameeleza kuwa soko hilo linawasaidia wabanguaji wenye mitaji midogo kushiriki kikamilifu kwenye biashara bila kushindana moja kwa moja na makampuni makubwa ya kimataifa, huku pia likirahisisha wakulima kuuza mazao yao na kupata malipo kwa wakati.

Aidha, amesema upatikanaji wa korosho bora kwa bei inayokubalika kupitia soko hilo unachochea ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani katika masoko ya kimataifa.

Hata hivyo, Marwa ametaja changamoto ya upatikanaji wa mitaji kuwa bado ni kikwazo kikubwa kwa wabanguaji wengi kutokana na gharama kubwa za uwekezaji katika vifaa na teknolojia.

“Ni muhimu Serikali ikaweka mazingira rafiki ya mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha wabanguaji kupanua shughuli zao na kuongeza ushindani,” amesema Marwa.