Dodoma. Tume ya Utumishi wa Umma imetaja makosa matano yanayojitokeza mara kwa mara katika utumishi wa umma na kuchangia kuibuka kwa migogoro kazini, baada ya kushughulikia rufaa na malalamiko 85 ya watumishi.
Makosa hayo ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma na taaluma, utoro kazini, uzembe unaosababisha hasara kwa Serikali au mwajiri, kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo, pamoja na vitendo vya kudhalilisha utumishi wa umma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatano, Aprili 22, 2026, jijini Dodoma, Kaimu Katibu wa tume hiyo, John Mbisso, amesema changamoto hizo zimebainika wakati wa uchambuzi wa rufaa na malalamiko yaliyowasilishwa katika mkutano wa tatu wa tume kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema katika rufaa zilizopokelewa, watumishi wanane walikubaliwa na kurejeshwa kazini bila masharti, huku 17 wakikubaliwa kwa masharti.
Kati yao, 13 wameamriwa kesi zao zisikilizwe upya, na wanne wamepunguziwa adhabu. Aidha, rufaa 27 zimekataliwa.
Mbisso amesema mkutano huo uliofanyika chini ya mwenyekiti wake, Hamisa Kalombola, umehusisha rufaa 60 na malalamiko 25 kutoka kwa watumishi wa umma.
Kwa upande wa malalamiko, amesema masuala yaliyotawala ni pamoja na kutopandishwa vyeo, kutolipwa stahiki, kuondolewa kazini bila kuzingatia sheria, kutorekebishwa kwa vyeo, kutobadilishiwa muundo wa utumishi baada ya kujiendeleza kimasomo, pamoja na kusimamishwa kazi bila kufuata taratibu za kisheria.
“Pia, mamlaka mbili za kinidhamu ziliitwa mbele ya tume kwa mujibu wa kifungu cha 12(1)(g) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, ili kupewa maelekezo baada ya kukiuka sheria, kanuni na taratibu katika kushughulikia mashauri ya nidhamu ya watumishi walio chini yao,” amesema Mbisso.
Ametoa wito kwa watumishi wa umma, waajiri, mamlaka za ajira na nidhamu kuzingatia sheria, kanuni na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuepusha vitendo vinavyosababisha migogoro isiyo ya lazima.
Aidha, amewataka waajiri kutekeleza kwa wakati maagizo na maelekezo yanayotolewa na tume, na kwa wale wanaokusudia kukata rufaa ngazi ya juu kwa Rais, kufanya hivyo kwa wakati ili kuepusha ucheleweshaji wa haki kwa watumishi.
Amesisitiza kuwa uzingatiaji wa sheria na taratibu katika utumishi wa umma ni msingi wa kulinda haki za watumishi na kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
