Arusha. Taasisi ya Tiba na Mifupa na Ubongo Muhimbili (Moi) imesema, ajali za barabarani zimeendelea kuongezeka ambapo wagonjwa kati ya asilimia 60 hadi 62 wanatokana na ajali za barabarani.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti Moi, Dk Joel Bwemelo akizungumza jijini Arusha leo Jumatano Aprili 22, 2026 katika mafunzo maalum ya usalama wa miundombinu ya barabara nchini kwa wahandisi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), wahandisi toka sekta binafsi na wadau wengine.
Amesema kuwa kwa kipindi kirefu kumeshuhudiwa ajali zikiongezeka na katika kitengo cha dharura kwenye taasisi hiyo wanapokea wagonjwa karibu 8,000 na asilimia kati ya 60 hadi 62 wanatokana na ajali za barabarani.
Ameongeza kuwa kwa sasa ajali za pikipiki (bodaboda) zimeongezeka na kuchangia asilimia 41 ya majeruhi hao.
“Wagonjwa hao wakifika kwetu mara nyingi huwa na majeraha makubwa ya kichwa, shingo, mgongo na mifupa mirefu,ni wagonjwa wanaopata majeraha makubwa, hali inayosababisha vifo au ulemavu wa kudumu,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, alisema wataalamu wa afya wameamua kutoka nje ya vyumba vya upasuaji na kushirikiana na jamii kutoa elimu ya usalama barabarani ili kupunguza ajali.
“Tunaendelea kuhamasisha wananchi kufuata sheria za usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kuepuka kuendesha wakiwa wamelewa, kwa mwendo kasi au wakiwa wamechoka, pamoja na kubeba abiria kupita kiasi.Ajali za pikipiki hazipungui kwa sababu watu wengi wanapenda kutumia usafiri huo kwani ni wa bei rahisi na haukai kwenye foleni,”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Profesa Riziki Shemdoe, amesema suluhisho la ajali za barabarani linapaswa kuanza kwenye usanifu wa miundombinu.
Amesema taasisi zinazohusiaka na ujenzi wa barabara zinapaswa kuhakikisha zinazingatia usalama tangu hatua ya usanifu ili kupunguza ajali za barabara.
“Barabara salama zinaanza kwenye ubunifu wake. Bila kuzingatia usalama katika hatua ya usanifu na ujenzi hatutaweza kupunguza ajali hizi,” amesema.
Ameeleza kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Tarura kutoka Sh900 bilioni mwaka 2025 hadi Sh1.2 trilioni kwa mwaka huu ili kuboresha miundombinu ya barabara.
“Sisi tuliokabidhiwa rasilimali hizi tunapaswa kuhakikisha tunajenga barabara zitakazopunguza idadi ya majeruhi wanaofika hospitalini. Mhakikishe barabara mnazosimamia zinahusisha usalama, tuboreshe alama za usalama barabarani.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Road Safety Initiatives (Tarsi), ambao ndiyo wameandaa mafunzo hayo, Maliki Barongo amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wahandisi na wadau wengine kuhakikisha usalama wa barabara unaanza tangu hatua ya usanifu.
Amesema taasisi hiyo isiyokuwa ya kiserikali inayojishughulisha na utoaji wa elimu ya usalama barabarani ili kuimarisha usalama ina dira ya kuifanya Tanzania isiyokuwa na majeruhi watokanao na ajali za barabarani na vifo.
“Sisi jukumu letu ni kuelimisha watanzania kuanzia wajenzi, madereva watumiaji wa barabara na tangu mwaka 2022 hadi sasa tumeshatoa mafunzo kwa wahandisi 800 kote nchini,”amesema
“Mafunzo haya yanahusisha wadau kutoka Tatura, Tanroads na sekta binafsi, yakilenga kuboresha mipango na utekelezaji wa barabara salama,”
Naye mkufunzi wa usalama barabarani, Mhandisi Ronald Lwakatare amesema kuna shida barabarani sababu ni nyingi kuna udhaifu wa binadamu kuna miundombinu kuna magari yenyewe yanaweza kuwa na hitilafu lakini kikubwa kwenye mafunzo haya wamelenga kwa ajili ya ujenzi na utunzaji wa barabara ili zijengwe na kuwa salama.
“Nia ni kuhakikisha kwamba msisitizo mkubwa tunaotoa kwa wahandisi ni kwamba suala la usalama barabara ianze tangu kwenye mipango na kusanifu barabara kuliko kusubiri baada ya kujenga ndipo tunaanza kuitikia matatizo yanapotokea,”amesema Lwakatare.
