Asimamishwa kwa tuhuma za kulazimisha wafiwa kununua majeneza yake

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure imemsimamisha kazi mtumishi wake katika Kitengo cha Mochwari baada ya kudaiwa kulazimisha wafiwa kununua majeneza kwake.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa hospitali hiyo, Elidaima Kimaro leo Jumatano Aprili 22, 2026 imesema mtumishi huyo alikuwa anauza majeneza hivyo kuwalazimisha wafiwa kununua kwake.

“Tumepokea taarifa ya mtumishi Kitengo cha Mochwari anayeuza majeneza na kulazimisha wafiwa kununua kwake na tayari umeshachukua hatua za haraka za kumsimamisha kazi mtumishi huyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo,” imesema taarifa hiyo.

Hospitali hiyo imewataka wananchi wanaokutana na changamoto ya aina hiyo kuwasiliana na hospitali kupitia namba za simu za viongozi zilizobandikwa kwenye mbao za matangazo hospitalini hapo.

Pia, wametakiwa kutoa taarifa kupitia masanduku ya maoni yaliyowekwa katika kila idara kwa ajili ya kupokea maoni, mapendekezo na changamoto yoyote kutoka kwa wananchi.

“Lakini pia unaweza kufika dawati la huduma kwa mteja lililopo ofisi ya mbele kabisa ya viwanja vya Hospitali hii kutoa maoni yako,”imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu (jina limehifadhiwa), baadhi ya wafiwa walilazimika kununua majeneza ya mtumishi huyo baada ya kuambiwa marehemu wao watachomwa dawa ya kutosha itakayomfanya akae muda mrefu hadi kuzikwa.

“Aliwahakikishia wafiwa endapo watanunua kwake jeneza angeushughulikia mwili wa marehemu wao kwa umakini mkubwa na heshima inayostahili…angeufanyia maandalizi yote muhimu, ikiwemo usafi, uvaaji na uhifadhi sahihi, ili kuhakikisha mwili unabaki katika hali nzuri hadi siku ya mazishi,”amesema.

Amesema baadhi waliambiwa angeutumia mchanganyiko wa dawa maalumu unaosaidia kuhifadhi mwili kwa muda mrefu bila kuharibika hasa kwa waliokuwa wanasafirisha.