Maswa. Wakati changamoto ya uhaba wa malisho ikiendelea kuathiri uzalishaji wa mifugo, Serikali na wadau wake wameibuka na mkakati mpya wa kuhamasisha wafugaji kuanzisha mashamba ya malisho, hatua inayotajwa kuwa mkombozi wa sekta ya mifugo na chanzo cha ongezeko la kipato kwa kaya.
Wito huo umetolewa Aprili 22, 2026 na mtaalamu wa malisho, William Mataba kutoka Sao Hill Industries, alipokuwa akitembelea shamba la mfano la mbegu za malisho katika kijiji cha Masela, wilayani Maswa, mkoani Simiyu.
Mataba amesema Serikali, kupitia miradi mbalimbali ikiwemo inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, inaendelea kuhamasisha wafugaji kubadili mtazamo na kuingia katika ufugaji wa kisasa unaozingatia ubora wa malisho badala ya wingi wa mifugo.
“Tunasisitiza wafugaji kufuga mifugo michache yenye tija kwa kuhakikisha wanakuwa na mashamba yao ya malisho. Hii ndiyo njia ya kupata mifugo yenye afya na kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama,” amesema Mataba.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zinaenda sambamba na ugawaji wa mbegu bora za malisho pamoja na uanzishaji wa mashamba darasa ili kuwajengea wafugaji uelewa wa mbinu bora za ufugaji na utunzaji wa mazingira.
Wafugaji wamepokea wito huo kwa mitazamo chanya, wakieleza kuwa uwekezaji katika mashamba ya malisho unaweza kubadili kabisa maisha yao.
Mfugaji Basu Kayungilo kutoka Meatu amesema ukosefu wa malisho ya uhakika umekuwa ukisababisha mifugo kudhoofika na hata kufa.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano akiongea na wafugaji wa mkoa wa Simiyu walioko katika mradi wa mabadiliko ya tabia nchi Simiyu juu umuhimu wa kuwa na mashamba malisho ya mifugo. Picha na Samwel Mwanga
“Shamba la malisho ni kama benki kwa mfugaji. Likisimamiwa vizuri, linahakikisha mifugo inapata lishe bora, uzalishaji unaongezeka na kipato kinakuwa cha uhakika,” amesema.
Kwa upande wake, Specioza Mikaeli kutoka Busega amesema wafugaji wengi bado wanategemea malisho ya asili ambayo hupungua wakati wa kiangazi, akitoa wito kwa serikali za mitaa kutenga maeneo maalum ya malisho na kuimarisha elimu ya ufugaji wa kisasa.
Naye Limi Kulwa wa kijiji cha Shishiyu, wilayani Maswa, amesema umuhimu wa kupanda na kuhifadhi nyasi bora hauwezi kupuuzwa, hasa katika kukabiliana na vipindi vya ukame vinavyoathiri uzalishaji wa mifugo.
“Lishe bora kwa mifugo ni msingi wa faida. Bila malisho ya uhakika, mfugaji anabaki na hasara,” amesema.
Sehemu ya shamba la mfano la malisho ya mifugo katika kijiji cha Masela wilaya ya Maswa lililotembelewa na wafugaji wa mkoa wa Simiyu walioko kwenye Mradi wa Mabadiliko ya tabia nchi Simiyu. Picha na Samwel Mwanga
Akizungumza kuhusu jitihada hizo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Vincent Naano, amesema ni wakati wa viongozi na wataalamu kushirikiana kubadilisha fikra za wafugaji ili kuendana na mahitaji ya uchumi wa sasa.
Ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana kuhakikisha upatikanaji wa malisho unakuwa wa uhakika, akisisitiza kuwa mageuzi katika sekta ya mifugo yanaweza kuwa chachu ya kuondoa umaskini na kukuza uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.