…..
NA: DK. REUBENI LUMBAGALA, TANGA
Moja ya ahadi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wake ni kuwawezesha kiuchumi kwa kujenga mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao. Pia, kuwawezesha kimitaji kufikia malengo yao ya kukuza biashara na ustawi wao kwa ujumla.
Hakuna ubishi kuwa maendeleo ya nchi yamebebwa kwa kiasi kikubwa na sekta binafsi. Unahitajika ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi (Public and Private Partnership – PPP) kufanikisha kasi ya maendeleo nchini.
Kwa kutambua umuhimu wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi na maendeleo kwa ujumla, serikali imeanzisha Kituo cha Sekta ya Umma na Binafsi ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya kimaendeleo kwa kuzingatia kuwa wadau hawa wawili – sekta ya umma na binafsi ni muhimu.
Wananchi kwa kutambua ukweli kuwa serikalini kuna ajira chache na sekta binafsi ndiyo injini ya maendeleo, kumekuwa na mwamko wa baadhi ya wananchi kujiajiri wenyewe ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao na kuchangia pato la Taifa kupitia ulipaji kodi serikalini.
Kwa mfano, biashara ya vyakula vilivyopikwa inayofanywa na mama na baba lishe katika sehemu mbalimbali nchini ni moja ya shughuli ambayo kama itawekewa mazingira mazuri na kufanyika kisasa zaidi, inaweza kuinua hali za maisha ya wananchi wengi na kuchagiza pato la Taifa.
Hii inatokana na ukweli kuwa huduma ya vyakula inahitajika maeneo mengi, mathalani: masokoni, vituo vya mabasi, migodini, maofisini, shuleni, hospitalini, baharini, na maeneo mengine kadha wa kadha.
Hivyo basi, ufanyikaji wa shughuli zao si tu unaongeza kipato kwao lakini pia unawezesha kufanyika kwa shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi zinazohitaji uwepo wa huduma ya vyakula.
Aprili 21, 2026, Rais Dk.Samia alihudhuria Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania, hafla iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Rais Dk. Samia aliahidi kushughulikia changamoto zao ikiwemo kupata sehemu nzuri za kufanyia biashara ili wafanye shughuli zao katika hali ya usafi na ubora zaidi.
Sanjari na hilo, Rais Dk. Samia aliikabidhi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hundi ya zaidi ya shilingi bilioni 94.1 ili zitumike kuwakopesha wajasiriamali wadogo wakiwemo baba na mama lishe. “Sitawaangusha, nitasikiliza changamoto zenu na kuzifanyia kazi,” alisema Rais Dk. Samia.
Baadhi ya mama na baba lishe wanakabiliwa na changamoto ya mitaji, hali inayosababisha kufanya kazi zao katika mazingira duni, hivyo kushusha heshima na thamani ya kazi hiyo.
Uwezeshaji wa fedha hizo ni dhamira njema ya Rais Dk. Samia ya kuhakikisha wajasiriamali hao wanafanya shughuli zao kwa ubora na kwa ufanisi ili nao wachangie maendeleo ya nchi.
Muhimu ni kwa viongozi wenye dhamana ya kusimamia fedha hizo, kuhakikisha zinawafikia walengwa nchi nzima bila upendeleo wala urasimu ili malengo ya Rais Dk. Samia ya kuwainua kiuchumi wajasiriamali hao iweze kutimia.
Mungu Ibariki Tanzania.
Maoni : 0620 800 462.

