JKU inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar imesema hivi sasa kila mechi kwao ni mapambano ya kusaka pointi tatu, huku ikikolezwa na ongezeko la bonasi kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar, Kanali Makame Abdallah Daima.
Kauli hiyo imetolewa na Kocha Msaidizi wa JKU, Hamis Hamad akisema bonasi hiyo ambayo hakuiweka wazi ni kiasi gani cha fedha, ni sehemu ya mkakati wa kufanya vizuri kwani imekuwa chachu na hamasa ya kuongeza juhudi kwao ndani ya uwanja.
Akizungumza baada ya mchezo kati yao na Zimamoto uliochezwa Aprili 12, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja na kushinda 2-1, kocha huyo amesema kwa sasa kwao kila mechi ni njia ya kufikia nafasi ya kusaka ubingwa.
Amesema kilichobaki kutoka kwao ni kuwaombea wapinzani wao wapotezea ili kuwarahisishia kazi ya kufika wanapohitaji.
“Mechi ni ngumu, lakini tunaamini tutashinda na tutachukua ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, tunashkuru Mkuu wa Jeshi kwa kuweka bonasi, tukishinda tunapata chetu bila mkopo,” amesema.
Ushindi huo umeifanya JKU kukusanya pointi 42 zilizoitoa nafasi ya nne hadi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar kwa tofauti ya pointi moja na kinara KVZ yenye 43, huku Fufuni ikiwa ya tatu ikikusanya pointi 41, huku zikisalia mechi nane kuhitimisha msimu huu.
