Mwandishi wa vitabu aiomba Tanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kukifanya Kiswahili lugha ya kufundishia

Dar es Salaam. Mwandishi nguli wa vitabu na mshairi, Abdilatif Abdalla ameisihi Serikali ya Tanzania, kwa heshima ya mchango wa Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere, kuangalia upya hatua za kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa chombo rasmi cha kufundishia shuleni, akisisitiza kuwa hatua hiyo inawezekana.

Amesema hata Kiingereza na lugha nyingine za Ulaya zilinyanyaswa na Kilatini, mfano, ilidaiwa kuwa Kiingereza hakina majina ya dawa na sayansi, na kwamba elimu bora ni ile inayofundishwa kwa Kilatini.

Abdalla mwenye asili ya Kenya, aliyasema hayo usiku wa jana, Jumatatu Aprili 14, 2026, jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.

Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuendeleza urithi wa fikra na maono ya Mwalimu Nyerere kupitia lugha ya Kiswahili na uandishi wa ubunifu.

“Kwa heshima ya Mwalimu Nyerere, kwa unyenyekevu mkubwa naiomba Serikali ya Tanzania ifikirie tena jambo hili; Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia katika shule zetu, inawezekana,” amesema.

Pia Abdalla ameiomba Serikali ya Tanzania kuifanya tuzo hiyo ihusishe mataifa mengine ya Afrika badala ya kuhusisha Watanzania pekee. Amesema hatua hiyo itaiwezesha tuzo hiyo kuendana na maono ya hayati Mwalimu Nyerere.

Akizungumzia uandishi bunifu, amesema ni muhimu katika kulea na kukuza jamii ili kuwe na misingi na misimamo thabiti.

“Uandishi bunifu ni kichocheo cha fikra za watu kuhusu hali za jamii zao. Uhai wa jamii yoyote hurutubishwa kwa kuwepo kwa machapisho yaliyoandikwa kwa lugha yake yenyewe,” amesema.

“Tujihimize sote tulio kwenye sanaa ya uandishi, hasa waandishi chipukizi, tujaribu kuwa waandishi bora zaidi kwa kujifunza mbinu mbalimbali za uandishi kutoka kwa waandishi waliobobea,” ameongeza.

Amesema ili waandishi wachanga wawe bora, ni lazima wawe na tabia ya kusoma ili kubuni mbinu na lugha mwafaka wa kisanii badala ya kuendelea kuiga lugha za wengine.

Akizungumzia tuzo hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo alisema hadi mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetumia Sh4.2 bilioni kugharamia tuzo hizo, ikiwa ni msimu wake wa nne.

“Fedha hizo ni kwa ajili ya uchapishaji wa vitabu, zawadi kwa washindi, na uwekezaji huu umesaidia kukuza sekta ya uchapishaji,” amesema.

Profesa Nombo amesema kwa miaka ijayo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itashirikiana na vyuo mbalimbali kuendesha warsha hizo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa fursa kwa waandishi wazawa ambao ni hazina kwa taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Profesa Penina Mlama alielezea mwitikio wa Watanzania katika tuzo hizo akisema jumla ya miswada 260 imepokelewa ikilinganishwa na miswada 282 iliyowasilishwa mwaka 2025.

Amesema kati ya miswada 260 iliyowasilishwa mwaka huu, 86 ilikuwa ya ushairi, riwaya 53, hadithi za watoto 73 na tamthilia 48.

“Tunafurahi kuona washiriki wametoka katika mikoa 27 ya Tanzania Bara na Visiwani, na hii inaashiria ushiriki wa maeneo yote ya nchi yetu. Pia tumepokea miswada kutoka kwa Watanzania waishio nje ya nchi,” alisema.

Kwa upande wa jinsia, Profesa Mlama alisema miswada 184 iliwasilishwa na wanaume huku 76 ikiwasilishwa na wanawake, akisisitiza kuwa changamoto kubwa iliyobainika ni baadhi ya washiriki kutotimiza vigezo.

Mshindi wa kwanza katika tuzo hiyo hupatiwa Sh10 milioni na ngao, pamoja na miswada yake kusambazwa shuleni. Mshindi wa pili hupata Sh7 milioni pamoja na cheti, na mshindi wa tatu hupatiwa Sh5 milioni pamoja na cheti, huku walioingia katika orodha teule wakipatiwa vyeti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dk Aneth Komba, amesema tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ina mchango mkubwa katika kufikia madhumuni ya jumla ya elimu ya mafunzo katika ngazi mbalimbali nchini.

Dk Komba amesema tuzo hizo humjengea mwanafunzi ubunifu, uwezo wa kufikiri kwa kina na kutatua matatizo, pamoja na kujenga umahiri wa kusoma, kujiamini na kutumia stadi za lugha ikiwemo Kiswahili.

Akizungumzia maboresho ya mitalaa, Dk Komba alitaja somo jipya lililoanzishwa ni fasihi ya Kiswahili, ambalo linalenga kuibua vipaji vya wanafunzi katika kubuni na kutunga kazi za kisanaa, ikiwemo mashairi, hadithi fupi, riwaya, maigizo, vichekesho na majigambo.

“Tuzo hizi ni nyenzo madhubuti inayochangia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, toleo la 2023, na mitalaa iliyoboreshwa ya 2023 kwa vitendo. Kwa ujumla, tuzo hii bunifu inaongeza maandiko bunifu katika shule,” amesema.

Katika tuzo hizo, washindi walikuwa ni John Hiluka katika riwaya iliyozungumzia waraka kutoka gerezani; upande wa ushairi mshindi alikuwa Abdallah Ngereza akiwa na muswada wa Muwinda Elimu.

Kwa upande wa hadithi za watoto, mshindi wa kwanza alikuwa Amina Mohamed akiwa na kazi iitwayo Shumi na Vitungule, huku upande wa tamthilia mshindi akiwa Hamis Kibari kwa muswada wa Mfalme wa Mabadiliko.