Mimba za utotoni zavuruga elimu ya wasichana Simiyu

Simiyu. Tatizo la mimba za utotoni mkoani Simiyu limeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa elimu ya wasichana, huku wengi wao wakilazimika kuacha shule na kupoteza ndoto zao za maisha.

Baadhi ya wakazi wa mkoa huo, wakizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 14, 2026, wamesema kuwa tatizo hilo linaathiri zaidi familia zenye kipato cha chini, hasa katika maeneo ya vijijini ambako uelewa kuhusu afya ya uzazi bado ni mdogo.

Msichana mmoja, Mary Jacobo (jina limehifadhiwa), mkazi wa Wilaya ya Maswa mkoani Shinyanga, amesema alilazimika kuacha shule baada ya kupata ujauzito alipokuwa kidato cha pili.

 “Nilikuwa nataka kuwa mwalimu, lakini sasa nipo nyumbani na mtoto. Nimepoteza kila kitu,” amesema.

James Elias ni mkazi wa mjini  Bariadi amesema  kuwa malezi duni na umasikini ni miongoni mwa sababu zinazochangia mimba za utotoni.

“Wazazi wengi hatuna muda wa kufuatilia watoto wetu. Wengine wanashawishiwa kwa pesa ndogo na wanaume wakubwa,” amesema.

Kwa upande wake, mwalimu wa shule ya sekondari wilayani Meatu, Shadrack Rodric amesema kuwa  tatizo hilo linaathiri hata ufaulu wa wanafunzi.

“Kila mwaka tunapoteza wasichana kadhaa kwa sababu ya mimba. Hii inapunguza idadi ya wanafunzi wanaohitimu na kuathiri matokeo ya shule,” amesema.

Naye Mandago Jisena mkazi wa Wilaya ya Itilima amesema kuwa  mimba za utotoni zina madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi.

“Msichana anapokatiza masomo, hupoteza fursa za ajira na maendeleo ya baadaye. Hii inaongeza mzunguko wa umaskini katika jamii,” amesema.

Ameshauri kuimarishwa kwa elimu ya afya ya uzazi mashuleni, pamoja na kuongeza ushirikiano kati ya wazazi, walimu na Serikali katika kupambana na mimba za utotoni.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amesema kuwa  juhudi zinaendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na tatizo hilo.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii na kuwachukulia hatua wanaohusika na kuwapa mimba wanafunzi. Lengo ni kulinda haki za mtoto wa kike,” amesema.

Asisitiza umuhimu wa wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi na ulinzi wa watoto wao ili kupunguza matukio hayo.