Asilimia 65.5 ya watoto hawana umahiri wa kusoma, kuhesabu

Dar es Salaam. Utafiti mpya uliofanywa na Shirika la Uwezo Tanzania mwaka 2025 unaonyesha asilimia 65.5 ya wanafunzi wenye umri wa miaka sita hadi 16 hawana umahiri wa kusoma na kufanya hesabu rahisi.

Utafiti huo uliofanyika nchi nzima umehusisha watoto wa umri huo walio shuleni na wale walio nje ya shule huku mikoa ya Rukwa, Simiyu, Manyara, Morogoro, Kigoma, Tabora, Lindi, Shinyanga Mtwara na Songwe ikiwa na hali mbaya zaidi.

Utafiti huo kwa mara ya kwanza umewasilishwa Aprili 10 na wataalamu kutoka Shirika la Uwezo katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao ukihusisha wadau mbalimbali wa elimu na waandishi wa habari.

Akiwasilisha tafiti hizo, Dk Aimtonga Amani alisema utafiti unaonyesha Tanzania imefikia asilimia 98 kuelekea lengo la asilimia 100 la udahili wa watoto shuleni wakati ambao umahiri katika kusoma na hisabati umeshuka

Amesema ukilinganisha na utafiti uliofanyika mwaka 2017, inaonyesha kuwa umahiri katika stadi hizo ulikuwa kwa asilimia 45 wakati ambao lengo la udahili lilikuwa kwa asilimia 78.

“Hivyo inaonyesha umahiri katika kusoma na hisabati umepungua kutoka asilimia 45 mwaka 2017 hadi asilimia 34.5 mwaka jana,” amesema.

“Tusiporekebisha uwezo wa kusoma mapema, mambo mengine yote katika mfumo wa elimu yanakuwa magumu zaidi na ya gharama kubwa kurekebisha baadaye. Kusoma ni ujuzi wa msingi unaofungua milango ya kujifunza katika masomo yote,” amesema.

Hili linabainishwa wakati ambao utafiti unaonyesha kuwa nafasi ya mtoto kumudu stadi za msingi inategemea kwa kiwango kikubwa na eneo analokulia.

Tofauti ya asilimia 61.2 kati ya Dar es Salaam na Rukwa, inaonyesha pengo kubwa la kimsingi katika fursa za elimu huku watoto wanaotoka katika kaya zisizojihusisha na kilimo wanakuwa na umahiri kwa asilimia 63.7%, huku wanaotoka katika kaya zinazotegemea kilimo umahiri wao ukiwa kwa asilimia 35.8.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 67.6 ya watoto wa Dar es Salaam walikuwa na umahiri katika stadi za kusoma na kuhesabu, wakifuatiwa na Kilimanjaro (asilimia 58.7), Njombe (asilimia 52.9), Iringa (asilimia 51.1) na Tanga yenye asilimia 46.9.

Kwa mikoa ambayo bado umahiri wake uko chini ni Rukwa ambapo asilimia 6.4, Simiyu (asilimia 14.9), Manyara (asilimia 17.4), Mororogo (asilimia 18) na Kigoma asilimia 18.9

Kutokana na hali hiyo, Dk Amani alisema: “Ni muhimu sana kuboresha ujuzi wa kusoma mapema kwa kiwango kikubwa kwa kuweka mkazo kwenye stadi za msingi za kusoma na hili lifanyike hasa katika kanda mahususi ili kushughulikia tofauti za kijiografia. Hilo litawekezana kwa kuziba pengo la rasilimali ikiwemo kuboresha upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada kwa wanafunzi.”

Akizungumzia suala hilo, Mtafiti wa elimu, Dk Muhanyi Nkoronko ingawa nchi imepiga hatua kubwa katika udahili yaani watoto wengi wamo madarasani kutokana na sera ya elimu bila malipo, lakini ubora umedumaa kwa kiasi fulani.

Jambo hili lina mwingiliano wa mambo kadhaa yanayosababisha watoto kuwepo shuleni lakini wasijue kusoma, kuandika, wala kuhesabu ikiwemo watoto kutoandikishwa kwa wakati, jambo linalosababuisha kushindwa kupata umahiri unaotakiwa.

Amesema wingi wa wanafunzi, ni jambo linalofanya walimu wasiweze kuwafikia kikamilifu na hili linachangiwa na uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kuwa mkubwa sana.

“Walimu wanalemewa na vipindi vingi na mzigo wa kusahihisha, hivyo wanajikita katika kumaliza mtalaa badala ya kuhakikisha umahiri unapatikana kwa mwanafunzi,” amesema.

Kukosekana kwa lishe na mazingira ya nyumbani nayo ni moja ya sababu inayofanya watoto wengi kuwa na njaa na tafiti zinaonyesha mtoto mwenye njaa hawezi kuelewa vema masomo.

“Ni wazi kuwa mtoto asiyeweza kumudu stadi za msingi ana uwezekano mkubwa wa kuacha shule au kushindwa kuendelea na elimu ya ngazi inayofuatia, hivyo tutakuwa na vijana wengi wasio na maarifa mtaani. Serikali inatumia fedha nyingi kufanya watoto wawepo shuleni lakini ikiwa watoto hao hawajifunzi, hivyo ni uwekeziji usio na tija. Ni wazi kuwa kusoma si kujifunza,” amesema.

Ili kuondokana na hali hiyo, ameshauri kuongezwa kwa uwekeziji katika elimu ya awali na msingi pamoja na kuajili walimu wengine zaidi, kuongeza madarasa na vifaa vya ufundishaji na ujifinzaji ili kupunguza uwiano kati ya mwanafunzi na mwalimu.

Kauli ya Dk Nkoronko inaungwa mkono na Mwalimu mstaafu, Leokadia Maswa anayesema watu wanavyozidi kupambana kupeleka watoto wao katika shule za binafsi, kinakauwa kiashirfia kuwa hawana imani na kile kinachotolewa kwenye shule za Serikali.

“Wakati wetu sisi shule za Serikali ndiyo zilikuwa zinasifiwa kwa kufanya vizuri, walimu wanajituma na kuhakikisha wanafunzi wanaelewa kwa kiwango kinachotakiwa, labda kwa sababu wanafunzi nao hawakuwa wengi kama sasa,” amesema.

Amesema ongezeko la wanafunzi lisiloendana na kasi ya uwekezaji ni miongoni mwa mambo yanayofanya walimu kushindwa kufanya kazi zao kikamilifu.

“Sera ya elimu bure ilikuja na mambo mengi sana, hali hii ilifanya hata wazazi kuacha kuchanga vitu vidogovidogo vilivyokuwa vinasaidia uendeshaji wa shule, matokeo yake kama ruzuku haitatolewa kwa kiwango kinachotakiwa mambo mengi yanakwama,” amesema.

Kuhusu ruzuku aliyosemwa Maswa, wadau wanasema ni wakati sasa wa kufanya mapitio ili kuhakikisha ubora wa elimu unaendana na mafanikio ya udahili yanayoshuhudiwa.

Wamesema kiwango fedha kinachotolewa kwa mwanafunzi kwa sasa hakiendani na ongezeko la maisha.

Kuhusu utoaji wa ruzuku, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake ya mwaka wa fedha 2024/2025 anaonyesha ruzuku ya elimu bila malipo kwa ajili ya shule za msingi na sekondari ilitolewa pungufu kwa kiasi cha Sh2.68 bilioni katika mamlaka za serikali za mitaa tisa kutoka kiasi kilichotengwa cha Sh13.46 bilioni.

Anasema upungufu huu unaweza kuathiri uendeshaji wa shule na ufundishaji wa wanafunzi kwa kuzuia upatikanaji wa vifaa muhimu vya kufundishia na kujifunzia.

Utoaji pungufu wa ruzuku za elimu bila malipo unachangiwa na hazina kushindwa kupeleka fedha kwa wakati na kwa kiasi kilichopangwa.

 “Napendekeza, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu -Tamisemi kuhakikisha kuwa fedha zilizoidhinishwa zinatolewa kwa wakati kwa mamlaka za serikali za mitaa kwa ajili ya kugharamikia utoaji wa elimu bila malipo ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule zote za serikali,” inasema ripoti ya CAG.

Kwa kutambua hali hii mwishoni mwa Januari 2026, Serikali ilizindua mpango mkakati wa kisayansi wa kujenga umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la pili ili kukabiliana na changamoto ya uwepo wa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma na kuhesabu.

Mpango mkakati huo utakaotekelezwa ndani ya miaka mitano unalenga, kuhakikisha kila mtoto anamudu stadi za msingi afikapo darasa la tatu kupitia njia za kisayansi, shirikishi na bunifu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema mkakati huo utakwenda kuimarisha ufundishaji kwa kufanya mafunzo endelevu kwa walimu na kusimamia namna bora ya kufundisha elimu ya awali, darasa la kwanza na pili.

“Pia, tutakuwa na maendeleo endelevu ya walimu ya kuwaandaa, kuwashirikisha hasa katika kuandaa vifaa vya kufundishia, tutahakikisha kunakuwepo na nyenzo za kufundishia na kujifunzia ambazo zinapatikana kila eneo nchini, miongoni mwake ni vizibo vya chupa za soda,” amesema.

“Mbali na hayo, utafanyika upimaji ili kuhakikisha mpango unaenda vizuri kama ilivyokusudiwa kupitia tathmini na upimaji.

“Mwisho ni ushirikishwaji wa wazazi, walezi na jamii kwa jumla wake. Sisi hatutaeleza mengi sasa hivi, tutakusikiliza lakini kuanzia hapa baada ya uzinduzi, tutakuwa tunaeleza, kusimamia na kufuatilia; na wenzetu wa Tamisemi,” alisema.