Dodoma. Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Ngwisa Mpembe ameiomba Serikali kuwapunguzia viwango vya riba ili kuiinua sekta hiyo na kukuza uchumi wa Taifa.
Ametoa wito huo leo Jumatano Aprili 15,2026 wakati wa mkutano kati ya Serikali na sekta binafsi ambapo pia wameomba ushirikiano kipindi hiki Taifa linatekeleza mpango wa dira ya 2050.
Mpembe amesema kwa muda mrefu, mashirika ya sekta binafsi wamekuwa na kilio cha riba ya tarakimu moja ili kupunguza gharama za kukopa na kukuza biashara ambayo ingesaidia kuongeza mapato na kukuza uchumi.
Amesema uwepo wa utitiri wa taasisi za sekta binafsi hausaidii kufikia malengo badala yake kiundwe chombo kimoja chenye nguvu.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali ina nia ya dhati ya kushirikiana na sekta binafsi ili kuendesha uchumi wa nchi.
Profesa Mkumbo ameahidi kuwa Serikali itaandaa mkutano mwingine siku za usoni ukiwakutanisha na sekta za fedha ili kuona jinsi ya kufikia kiwango cha riba walau tarakimu moja.
Amesema kuwa sekta ya umma na binafsi inahitaji kuwa wabunifu wa suluhu za biashara na uwekezaji na hakuna sababu ya kugombana wala kuvutana wakati wote wana nia moja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mabenki Tanzania, Tusse Joune amesema ili kufikia malengo ya Dira ya 2050, Tanzania inahitaji sekta imara itakayowezesha wananchi wengi kupata huduma za kibenki.
Amesema mkakati wa Taifa kwa sasa ni Sekta binafsi kuchangia uchumi wa nchi kwa asilimia 70, ambapo ili ufanikiwe pande zote zitaimba wimbo mmoja na kukubaliana kwa pamoja nini kifanyike.
