Watuhumiwa 53 wakamatwa na Polisi Iringa

Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewakamata watuhumiwa 53 wanaodaiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu, kufuatia operesheni maalumu iliyoanza Aprili 1, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 15, 2026  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,  Allan Bukumbi, amesema operesheni hizo zinalenga kudhibiti uhalifu na kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaendelea kuwa shwari mkoani humo.

 “Kuanzia Aprili Mosi, 2026, tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 53 wa makosa mbalimbali ambao tayari wamefikishwa mahakamani,” amesema Kamanda Bukumbi.

Kamanda Bukumbi amesema baadhi yao tayari wamehukumiwa vifungo jela kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo kujeruhi, wizi, shambulio, kutishia kuua na uvunjaji.

Katika operesheni hizo, Jeshi la Polisi pia limesema limefanikiwa kukamata mali zinazodaiwa kuwa za wizi zikiwemo pikipiki tano, majiko ya gesi saba, luninga tano, bajaji moja, kompyuta aina ya Dell na microwave moja.

Miongoni mwa waliokamatwa ni Ramadhani Mussa (33), dereva mkazi wa Dar es Salaam, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kubainika kutoa taarifa za uongo kuwa aliibiwa sehemu zake za siri.

Wengine waliotajwa ni Mussa Kaundi (39), mfanyabiashara mkazi wa Mafinga, pamoja na wenzake wawili kutoka Isakalilo na Usokami, ambao kwa nyakati tofauti walidai kuibiwa sehemu za siri.

Hata hivyo, uchunguzi wa kitabibu ulibaini kuwa madai hayo hayakuwa ya kweli na kesi zao zimekamilika tayari kwa kufikishwa mahakamani.

“Baada ya uchunguzi wa kitabibu kufanyika, watuhumiwa hao walibainika kutoa taarifa za uongo na upelelezi wa kesi zao umekamilika.”