Mbeya City yaachana na Maxime baada ya siku 130

UONGOZI wa Klabu ya Mbeya City, umetangaza kufikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba wa Kocha Mecky Maxime pamoja na wasaidizi wake ambao ni Nizar Khalfa (Kocha Msaidizi) na Francis Mkanula (Kocha wa Utimamu wa Mwili).

Uamuzi huo umefanyika Aprili 16, 2026 ikiwa ni saa chache baada ya Mbeya City kupokea kipigo cha mabao 6-0 kutoka kwa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

“Tunatambua na kuthamini jitihada walizofanya katika kuboresha utendaji wa timu yetu na tunamshukuru kwa mchango wake uliotukuka kwa kipindi chote alichoongoza timu yetu.

“Tunamtakia Kocha Mecky Maxime na wasaidizi wake kila la kheri,” imesema taarifa hiyo kwa umma iliyotolewa leo Aprili 16, 2026 na uongozi wa Mbeya City FC.

Maxime anaondoka Mbeya City baada ya kudumu kwa takribani siku 130 ambazo ni sawa na miezi minne na siku tisa tangu alipotambulishwa Desemba 7, 2025, akichukua nafasi ya Malale Hamsini.

Maxime ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa Dodoma Jiji huku pia akiwahi kuzinoa Ihefu (sasa Singida Black Stars) na Mtibwa Sugar, alisaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia Mbeya City maarufu Wagonga Nyundo wa Mbeya.

Wakati Maxime anatua Mbeya City, aliikuta timu hiyo inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa imecheza mechi kumi na kukusanya alama nane.

Hata hivyo, Maxime hakuwa na matokeo mazuri kwani ameiacha Mbeya City ikishuka nafasi moja kutoka 12 hadi ikiangukia 13 na alama zake 17, na kufanya kocha huyo kuchangia pointi tisa katika mechi tisa alizoiongoza akiwa na wastani wa kupata pointi moja kila mechi. Jumla Mbeya City imecheza mechi 19 za Ligi Kuu Bara na kukusanya alama 17.

Mechi tisa alizoongoza Maxime ndani ya Mbeya City, timu hiyo imeshinda mbili dhidi ya TRA United (2-0) na KMC (3-2), huku sare ni tatu dhidi ya Pamba Jiji (1-1), Dodoma Jiji (1-1) na Azam (0-0), ikipoteza nne dhidi ya Mtibwa Sugar (2-1), Fountain Gate (1-0), Singida Black Stars (4-1) na Yanga (6-0).

Wakati Maxime akiondoka Mbeya City, msimu huu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu Bara, imeshuhudiwa makocha 15 wakiachana na timu kwa sababu mbalimbali ikiwemo matokeo yasiyoridhisha au kupata dili sehemu nyingine.

Walioachana na timu kwa makubaliano ya pande mbili kwa kile kilichoelezwa ni matokeo yasiyoridhisha ni Dimitar Pantev (Simba), Abdallah Mohamed ‘Bares’ (KMC), Marcio Maximo (KMC), Ally Mohamed Ameir (Coastal Union), Mohamed Muya (Coastal Union), David Ouma (Singida Black Stars), Zedekiah Otieno (Tanzania Prisons), Salum Mayanga (Mashujaa), Romain Folz (Yanga), Malale Hamsini (Mbeya City), Mohamed Ismail ‘Laizer’ (Fountain Gate) na Mecky Maxime (Mbeya City).

Kwa upande wa Fadlurahman Davids aliachana na Simba baada ya kupata dili Raja Club Athletic ya Morocco, huku Miguel Gamondi akitua Taifa Stars akitokea Singida Black Stars, wakati Dennis Kitambi akiachana na Fountain Gate alipoamua kujiweka pembeni kwa sababu zake binafsi.