Bilionea Laizer aipatia shule ya Makiba mashine ya kudurufu

Arumeru. Mchimbaji maafuru wa madini ya Tanzanite Saniniu Laizer ameipatia Shule ya Sekondari Makiba ya wilayani Arumeru mkoani Arusha mashine ya kudurufu yenye thamani ya Sh4 milioni.

Bilionea Laizer akizungumza kwenye mahafali ya 15 ya kidato cha sita yaliyofanyika katika Kijiji cha Makiba Aprili 17, 2026 amesema ametoa mashine hiyo kama zawadi ya maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.

Amesema hatua hiyo ni kuunga mkono suala la elimu kwa kuwa ndiyo inaendesha mambo yote hivi sasa duniani.

Mkuu wa shule hiyo, Paul Kimaro amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1996 kwa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na ikasajiliwa mwaka 1997. Shule hiyo ina wanafunzi 636 na walimu 50.

Makamu Mwenyekiti wa shule ya sekondari Makiba ya wilayani Arumeru mkoani Arusha, Hamis Kimu akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 30 na mahafali ya 15 ya kidato cha sita ya shule hiyo. Picha na Joseph Lyimo

“Tumejenga mabweni mapya, maabara ya kisasa, maktaba iliyoboreshwa na matumizi ya Tehama katika ufundishaji, hatua inayosaidia wanafunzi kwenda na ulimwengu wa kidijitali,” amesema Kimaro.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Hamis Kimu ameeleza kuwa shule hiyo imepiga hatua hasa upande wa taaluma, kwani imekuwa na ufaulu mzuri kwa ngazi ya mkoa na wilaya.

Mmoja wa wanafunzi wa kidato cha sita wa shule hiyo, Bareri Jumanne amesema nidhamu ya wanafunzi inaendelea kuimarika kutokana na ushirikiano mzuri wa walimu, wazazi na wanafunzi.

Kutokana na hilo, amesema wanatarajia ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi wote wanaotarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita.

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Makiba ya wilayani Arumeru mkoani Arusha wakiwa kwenye maadhimisho ya miaka 30 tangu ianzishwe na mahafali ya 15 ya shule hiyo. Picha na Joseph Lyimo

Mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa chama cha wafanyabiashara wa madini Tanzania (Chammata), Mokia Ole Mrefu aliyehudhuria mahafali hayo amewatakia kila la heri wanafunzi ambao wanatarajia kufanya mitihani yao ya kuhitimu kidato cha sita hivi karibuni.