Pemba. Bweni la wasichana 167 la Skuli ya Sekondari ya Fidelcastro Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba, limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Ijumaa Aprili 17, 2026 huku wanafunzi 29 wakilazwa kutokana na mshtuko.
Wakizungumza baada ya kutokea moto huo baadhi ya wanafunzi wamesema moto ulianzia chumba cha wanafunzi wa kidato cha tano na kutakiwa kutoka kujiokoa kunusuru uhai wao na baadhi ya mali ingawaje hakuna mali yoyote iliyookolewa.
Wamesema waliona mripuko wa moto bila lya kufahamu chanzo chake ni kiti gani na kukimbilia nje kujinusuru.
Mkuu wa wa sekondari hiyo, aliyekuwepo katika tukio Seif Hamad Khalfan amesema walijaribu kupambana kupunguza madhara lakini walishindwa kuudhibiti huku wakiwa tayari wameshawapigia Zimamoto.
Amesema saa 2: 00 usiku wakati wanatoka msikitini wameona bweni linawaka bila ya kujua chanzo ni kitu gani.
“Mnamo majira ya Saa mbili usiku mara baada ya sala ya ishaa tuliona bweni la wanawake linawaka moto wanafunzi wote wakatoka nje hakuna alodhurika ispokuwa vifaa vyao kama mabuku,vitabu na magodoro na nguo zao “amesema.
Ofisa mdhamin Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohammed Nassor Salim amewanasihi wazazi waliofika kuonana na Watoto wao kuwa watulivu huku akiwahakikishia kutoa usimamizi wa kina na Wanafunzi hao wakiwekwa sawa kisaikolojia ili kurudi katika masomo yao .
Katika hatua nyingine Kamishna msimamizi wa kikosi cha zimamoto pemba Salama Pandu Khamis amesema moto ulikuwa mkubwa na kulazimika kutumia magari matatu ya maji kufanikisha uzimaji wa moto huo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid ameelezea kusikitishwa na tukio hilo na kuwaomba wazazi kuwa na subira, huku Serikali ikiendelea kufanya uchunguzi wa kilichosababisha kuungua kwa bweni hilo.
